Saturday, December 27, 2014

MKE WA TYSON ASHINDA MIRATHI

Mke wa muandaaji mahiri wa filamu George Tyson, Beatrice Shayo.
Stori: Mayasa Mariwata na Hamida Hassan
MKE wa muandaaji mahiri wa filamu George Tyson, Beatrice Shayo amefanikiwa kushinda kesi na kuwa msimamizi wa mirathi baada ya mtafaruku mkubwa uliotokea wa kugombea mali na mwanadada aliyekuwa akiishi na msanii huyo kipindi cha mwisho cha uhai wake, Lucy Sepetu.
Akizungumzia ishu hiyo Beatrice alisema anashukuru Mungu amempigania maana ndugu wengi wa mume hawakuwa upande wake, wengi wao walimuunga mkono Lucy lakini Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imempitisha kuwa msimamizi wa mirathi.
“Nililia sana na kumuomba Mungu kila kukicha kutokana na hili, nashukuru nimeshinda kesi na kuwa msimamizi wa mirathi yakiwemo mashamba, kiwanja, magari mawili na akaunti benki na hivi vyote navisimamia kwa ajili ya watoto wake watatu, ambao ni mwanangu, wa Monalisa na mwingine ambaye aliibuka baada ya kifo cha mume wangu,” alisema Beatrice.