Monday, December 22, 2014

STEVE NYERERE AANIKA SABABU ZA KUJITOLEA MSIBA WA AISHA

STAA wa filamu za Kibongo, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ amesema anakumbuka fadhila za marehemu Mwanaisha Mohamed Mbegu ‘Aisha Madinda’ ndiyo maana amejitoa kwa hali na mali katika msiba wake kwani anawaonea huruma watoto wake ambao aliishi nao kama kaka yao enzi za marehemu alipokuwa na uhusiano na mdau wa Muziki wa Dansi Bongo, Fikiri Madinda.
Staa wa filamu za Kibongo, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’(kulia) akijadili jambo na 'Lwiza Mbutu' kwenye msiba wa marehemu Aisha Madinda.
Akipiga stori na mwanahabari wetu, Steve alisema kuwa wakati anaanza kazi alipokelewa na  Aisha ambaye alimpeleka kwa Fikiri Madinda na kumtambulisha ambapo alikaa chini yao kwa muda wa mwaka mmoja.
“Msiba huu kwangu ni mkubwa nitamkumbuka daima Aisha kwa mazuri yake siwezi kulipa fadhila lakini kwa msiba huu nitachangisha kwa hali na mali ili tu tumsitiri dada yetu,” alisema Steve ambaye aliendesha kampeni ya kuchangisha rambirambi kwa kushirikiana na viongozi wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Marehemu Aisha aliyefariki katikati ya wiki iliyopita, alizikwa Ijumaa iliyopita nyumbani kwao Kigamboni jijini Dar.