Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amevunja ukimya akisema ni kweli alipokea Sh40.4 milioni kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP, James Rugemalira zikiwa matoleo ya kusaidia uendeshaji wa kanisa.
Askofu Nzigilwa ni mmoja wa watu waliopata fedha kutoka kwa Rugemalira anayehusishwa kugawa kwa watu mbalimbali mabilioni ya shilingi yanayohusishwa na fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow wakiwamo wabunge, mawaziri na viongozi wa dini.
Tayari baadhi ya viongozi wa Serikali wamewajibika kwa ama kutumia vibaya madaraka yao au kupokea fedha hizo kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Kupitia taarifa yake ya kurasa tatu kwa vyombo vya habari, Askofu Nzigilwa alielezea uhusiano wake na familia ya Rugemalira ulivyoanza na jinsi ambavyo amekuwa akitoa sadaka na michango mbalimbali ya hali na mali.
“Kanisa linategemezwa na nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliongoza kupitia michango ya watu. Hivyo, kwa waumini kutoa michango na matoleo kwa kanisa na watumishi wake ni jambo la kawaida katika desturi za imani yetu tangu nyakati za mitume,” alisema askofu huyo.
Alisema uhusiano wake na familia ya Rugemalira ulianza mwaka 2008 alipopangiwa katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu, Makongo Juu akiwa Paroko Msaidizi, Rugemalira akiwa muumini katika parokia hiyo.
Alisema akiwa katika parokia hiyo, walikuwa na ujenzi wa nyumba ya mapadri na mikakati ya ujenzi wa kanisa jipya la parokia hiyo na katika shughuli zote hizo, Rugemalira na waumini wengine walikuwa ni wachangiaji wazuri.
“Hata baada ya kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi tumekuwa tunashirikiana na kuwasiliana na familia ya Rugemalira katika masuala mbalimbali ya kikanisa na kijamii,” alisema.
Mamilioni yaingia
Kuhusu fedha hizo, Askofu Nzigilwa alisema katika moja ya mawasiliano yao Februari mwaka jana, Rugemalira alimuomba namba ya akaunti yake ya Benki ya Mkombozi ili aweke matoleo yake... “Kwa kuniomba akaunti hiyo nilijua anataka kuweka matoleo ya fedha; lakini kiasi alichokuwa amenuia kukiweka sikukijua mpaka nilipoangalia Bank Statement na kuona kampuni ya VIP Engineering imeingiza Sh40.4 milioni katika akaunti hiyo Februari 27, 2014.
“Niliwasiliana na Ndugu Rugemalira na kumwambia nimeona kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yangu; naye akaniambia hayo ni matoleo ambayo anaamini yatasaidia katika shughuli zetu za kitume na kichungaji. Nikamshukuru kwa ukarimu huo mkubwa,” alisema.
Alisema matoleo hayo yalipokewa kwa moyo mnyofu kutoka kwa mtu anayefahamika kwa ukarimu wake katika kusaidia Kanisa na watumishi wake.“Biashara na kampuni anazomiliki Rugemalira kwa mujibu wa sheria za nchi haviwezi kumpa shaka mtu anayemfahamu uwezo wake au kampuni yake kutoa mchango mkubwa kama huo.”
Kazi za matoleo
Huku akisema tangu apokee fedha hizo hakuna mamlaka yoyote iliyowahi kumhoji Askofu Nzigilwa alisema matoleo ya waumini hutumika katika shughuli na uendeshaji wa jimbo, parokia na taasisi zake; katika miradi maalumu iliyokusudiwa na pia kwa kadri ya matakwa na lengo la mtoaji.