Thursday, January 15, 2015

HAKUNA MGOMBEA URAIS ATAKAYEFARIKI NABII


Nabii John Komanya.

Wagombea wa urais wametakiwa kutokuwa na hofu juu ya tabiri mbalimbali zinazotolewa na watabiri wa nyota nchini kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.

Rai hiyo imetolewa na Mtumishi wa Mungu, Nabii John Komanya wa Nyumba ya Furaha Kiluvya Gogoni katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Mtumishi John alisema kufuatia tabiri zilizotolewa juu ya mgombea wa nafasi ya urais kuanguka jukwaani na kufa sambamba na kifo cha mwandishi wa habari siyo za kweli.

Alisisitiza kuwa suala la uchaguzi wa kiongozi yupi anayefaa kushika madaraka ya kuongoza nchi ni siri ya wapigakura wenyewe hata kama watabiri watabainisha sifa mbalimbali za kuvutia.

Pia alisema kuwa sifa za raisi mtarajiwa zilizotolewa kuwa atakuwa kijana na mwenye dini mbili si za kweli na kuwataka wale waliovuka rika la ujana kuchukuwa fomu ili waweze kufanikisha malengo yao ya kuwatumikia wananchi.

Aliongeza kuwa watabiri waliosema hayo wana sababu zao na kuwatisha wapigakura wasiweze kuwachagua wale wanaowaamini kuwa wanaweza kuwaongoza.

“Mungu huteua kulingana na moyo, utayari na msimamo wa kuweza kulitumikia taifa husika sambamba na utashi wa kuiongoza Tanzania na wala haangalii sura, mwili wala dini ya mgombea,” alisema.

Aidha, alikanusha pia taarifa za kuwapo kwa vurugu nchi nzima wakati wa uchaguzi na kubainisha baadhi ya mikoa itakayokuwa na maelewano hafifu ikiwamo ya Dar es salaam, Mara, Arusha, Mwanza, Morogoro Shinyanga, Mbeya Kigoma pamoja na Zanzibar.

Aliwakumbushia Watanzania kuzidisha maombi ili kufanikisha kupata kiongozi bora na siyo bora kiongozi.

Hii inatokana na utabiri uliotolewa jijini Dar es Salaam na  Maalim Hassan Hussein, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mtabiri maarufu nchini, marehemu Sheikh Yahya Hussein, aliyetabiri mambo 18 yatakayotokea mwaka huu wa uchaguzi,  likiwemo la kufariki ghafla wakati akipelekwa hospitali kwa kiongozi mmoja mzee ambaye yumo kwenye mchakato wa kugombea, sambamba na  mwandishi mmoja mashuhuri nchini atakufa kifo chenye utata kitakachoitesa Serikali na familia yake katika kutafuta sababu za kifo chake.
  
CHANZO: NIPASHE