Thursday, January 15, 2015

WALALAMIKIA WATOTO WAO KUHUSISHWA NA 'PANYA ROAD'

Idadi ya vijana wanaojihusisha na kundi  uhalifu maarufu kama ‘Panya Road’ waliokamatwa imeongezeka kutoka  1,391  kufikia 1,438 jijini Dar es Salaam huku baadhi ya wazazi na wakazi  wa Magomeni na Mwenge wakilijia juu Jeshi la Polisi kwa madai kuwa operesheni hiyo inawahusisha wasiohusika.


 Idadi hiyo imeongezeka  katika mkoa wa kipolisi Temeke ambapo kwenye operesheni ya juzi wahalifu hao walikamatwa 47 na kuongeza idadi ya kufikia 1,4 38.

Aidha vijana hao walikamatwa ni pamoja na wapiga debe katika vituo vya daladala, wacheza kamari, wavuta bangi, watumiaji wa dawa za kulevya na watumiaji wa gongo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa  kipolisi Temeke, Kihenya Kihenya, alisema juzi waliwakamata vijana 47 ambapo idadi Kamili inafikia 289.

Hata hivyo NIPASHE iliwatafuta Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Ilala, Mary Nzuki, simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokelewa na Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura, alituma ujumbe wa meseji uliosema  yupo kwenye kikao.

Joyce Mbaruku, mkazi wa Magomeni akizungumza na NIPASHE, alisema  operesheni hiyo inayofanywa na Jeshi la Polisi ni ya uonevu kwani wanakamata watu hovyo bila ya kufanya uchunguzi na kuwahusisha  na kundi la ‘Panya road’.

Alisema  ameshangazwa na taarifa za kukamatwa kwa vijana wake wawili huku wakihusisha na kundi hilo kwani tabia za watoto wake anazijua vizuri na  katika mtaa huo walipokamatiwa ni wageni na hawajawafahamu vizuri wenyeji wa mtaa huo.

“Taarifa hizi za kukamatwa kwa watoto wangu nimezipata kwa masikitiko makubwa sana kwani vijana wangu katika mtaa huu ni wageni  ni juzi tu tumeamia kutoka Shekilango hivyo Jeshi la Polisi linatakiwa kufanya upelelezi kwanza ili kuwabaini watu wanaowatafuta na kuwakamata,” alisema.

Filibert Mboya, mkazi wa Mwenge, ameshangazwa na operesheni hiyo kwa kusema vijana wengi waliokamatwa hasa katika maeneo ya Mwenge hawahusiki na kundi hilo la uhalifu.

Alisema rafiki zake watatu pamoja na mtoto wa kaka yake walikamatwa katika uwanja wa mpira Mwenge wakiangalia mazoezi ya mpira wa miguu ndipo Polisi walipotokea na kuanza kuwakamata.

“Watu waliokuwepo uwanjani baada ya kuona polisi walikimbia sana kwani walipiga risasi za moto mbili juu na nyingine za mabomu hivyo  wapita njia na watu waliokuwapo uwanjani hapo walishikwa na butwaa na kuanza kukimbia kila kona hivyo ndugu zangu hao wakakamatwa kutokana na kuzidiwa na moshi wa bomu la machozi,” alisema Mboya.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, alisema siyo ya kweli kwani operesheni hiyo inaendeshwa kwa kufuata taratibu zote na taarifa za vijana wanaokamatwa zinatoka kwa wazazi wao.

Aliongeza kuwa kama kuna watakaobainika kutohusika tawaachiwa huru.

chanzo: nipashe