Friday, February 6, 2015

MUSWADA WA MAHAKAMA YA KADHI WAONDOLEWA BUNGENI

Muswada wa Sheria ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara hautajadiliwa katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma baada ya serikali kuuondoa kwa maandalizi zaidi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema jana usiku kuwa wameamua kuuondoa muswada huo ili kupata fursa ya kutoa elimu zaidi kwa viongozi wa dini na kuufanyia marekebisho baadhi ya maeneo.

Alisema serikali inatarajia kuurejesha tena bungeni mwezi ujao. Hata hivyo, habari za uhakika kutoka Dodoma zinasema kuwa kulikuwa na mvutano mkali ndani ya kamati ya Bunge iliyokuwa inashughulikia muswada huo uliokuwa kwa misingi ya imani hivyo busara ilitumika kuahirishwa uwasilishwaji kwa mara ya pili kwani mjadala kwenye Bunge zima ungeweza kuleta mpasuko.

Muswada huo ulikuwa unawasilishwa kutokana na ahadi ya serikali kwenye Bunge Maalum la Katiba ambako mjadala ulikuwa mzito baadhi ya wajumbe wakitaka mahakama ya kadhi iingizwe kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akashauri kutungwa kwa sheria ya mahakama hiyo, badala ya kuuingiza kwenye katiba.

Tangu serikali itangaze kuwa itawasilisha muswada huo bungeni, kumekuwa na mvutano ndani ya jamii, kundi moja likiupinga kwa madai kuwa serikali haipaswi kujihusisha na masuala ya dini kama katiba inavyoelekeza. Ilielezwa kwamba kama Waislamu wanahitaji mahakama hiyo, basi waunde kwa njia zao wenyewe bila kuhusisha serikali.

Hata hivyo, serikali ilisema kuwa imeandaa muswada huo ili kuweka utaratibu wa kuundwa kwa mahakama hizo kisheria, lakini suala la uendeshaji wake na gharama hazitabebwa na serikali bali Waislamu wenyewe.

Tayari jumuiya za Kikristo kupitia maaskofu wao wamekwisha kutoa msimamo wao juu ya mahakama hizo wakisema kuwa siyo jukumu la serikali kuzianzisha.