Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda amesema kuwa ni halali na ni sahihi kutumia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari (watoto wa shule) katika shughuli za kisiasa.
Pinda ametoa kauli hiyo katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali ya mbunge wa viti maalum CHADEMA na Waziri kivuli wa Elimu Suzan Lymo aliyetaka kauli ya serikali kuhusiana na CCM kuwatumia wanafunzi wa shule za msingi katika sherehe za chama hicho zilizofanyika Februari 1, 2015 mjini Songea.
Akijibu swali hilo, Pinda amesema huo ni utaratibu halali wa Chama cha Mapinduzi ambao unaendena na mfumo wa uendeshaji wa chama hicho unaoanzia katika ngazi za chini kabisa.
Amesema 'Mtoto wa Nyoka ni Nyoka' hivyo watoto wanaotumika katika sherehe hizo, wazazi wao pia ni wanachama wa CCM, kwahiyo watoto hao wanapata mafunzo na malezi ya CCM kutoka kwa wazazi wao.
Amesema kuwatumia watoto hao hakuna madhara yoyote kwao kwani umri wao hauwaruhusu kufikiria masuala ya kisiasa.
“….Ni halali kwa kuwa wale ni watoto ambao bado hawajawa na uelewa wa masuala ya siasa wanachofurahia pale ni ile Parade tu tena ilipendeza kweli kwa sisi tuliokuwepo tulifurahia sana……Nimesema hili suala ni utaratibu wa CCM hakuna haja ya kubishana hapa……”Amesema Pinda.
Aidha mbunge Moses machali ameomba mwongozo akidai kuwa ana barua ( Iliyowekwa hapo juu ) inayoonesha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akiwalazimisha wanafunzi wa shule ya Songea Boys kuvaa sare na CCM na kwenda kwenye sherehe hizo, ambapo ametaka Waziri Mkuu afute kauli yake.
Akijibu mwongozo huo, Spika Makinda amesema kuwa hawezi kumlazimisha Waziri Mkuu kufuta kauli yake.