Friday, March 27, 2015

ZITTO AMETUSALITI

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Zuberi Kabwe ambaye ametangaza rasmi kuwania ubunge katika majimbo mengine, amelaumiwa na waliokuwa wapigakura wake waliodai amewaacha kwenye mataa, Uwazi Mizengwe limedokezwa.
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Zuberi Kabwe.
Zitto ametangaza kwamba atagombea ubunge kwa tiketi ya chama cha ACT- Tanzania katika majimbo yafuatayo ambayo majina ya wabunge na vyama vyao yamewekwa kwenye mabano; Kahama (James Lembeli, CCM), Kawe (Halima Mdee, Chadema), Segerea (Dk. Makongoro Mahanga, CCM) na Kasulu (Moses Machali, NCCR).
Kwa mujibu wa Zitto, majimbo hayo na mengine manne ambayo hajayataja anaweza kugombea na akapata kura nyingi na kushinda na ndiyo maana alipokuwa akiliaga bunge wiki iliyopita, aliwaambia wabunge kuwa watakutana tena ukumbini humo Novemba, mwaka huu.
Novemba uchaguzi mkuu utakuwa umekwishafanyika na ni wakati ambao wabunge watatakiwa kwenda kuapishwa bungeni.Baadhi ya wapigakura wa Kigoma Kaskazini waliozungumza na gazeti hili, walisema kwamba Zitto amewaacha kwenye mataa kwa sababu kama kweli amefanya vema katika jimbo lake litakuwa ni jambo la ajabu kulihama na kwenda kuongoza kwingine.
“Ukweli ni kwamba ametushangaza. Zitto amekimbia jimbo lake la Kigoma Kaskazini kwa nini? Hajatoa sababu ya msingi, kulikoni?” alihoji Ally Said Ally aliyejitambulisha kwa simu ya kiganjani kama mpigakura wake wa Kigoma.
Mwigulu Nchemba.
“Kuna ukweli anauficha, lazima kuna sababu za msingi zinazomfanya kukimbia jimbo lake. Katika jimbo hili kuna matatizo mengi ambayo hajayatimiza ndiyo maana ametuacha kwenye mataa,” alisema mpigakura mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Mohammed.
Tamko hilo tayari limewapa kiwewe wapambe wa wabunge wa majimbo hayo na hata wabunge wanaokalia viti hivyo na kuwafanya wajiandae kupambana na Zitto ikiwa ataibukia katika majimbo yao ya uchaguzi.
“Tutapambana na ajue kwamba tutawaeleza wapigakura wetu kuwa mtu huyu hafai na ndiyo maana amefukuzwa Chadema na kukimbia jimbo lake,” alisema mbunge mmoja ambaye jimbo lake limetajwa na Zitto kwamba anaweza kugombea.
Mbunge huyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa sasa kwa sababu Zitto hajasema wazi kama atakwenda katika jimbo lake alisema atasema mengi jimboni mwake ikiwa atatangaza rasmi na siyo ‘jumlajumla’ kama alivyofanya sasa.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao hivi karibuni,  Zitto ambaye amejiunga na chama cha ACT alisema atagombea nafasi ya ubunge kwa kuwa umri wake haumruhusu kugombea nafasi ya urais na kwamba jimbo atakalogombea litawekwa wazi baada ya yeye kushauriana na washauri wake kwa kuwa majimbo zaidi ya sita nchini yanamtaka agombee.
“Nitasema hapo baadaye nitagombea jimbo gani kwa sababu majimbo mengi yananiita nikagombee, Kawe wanatitaka, Segerea, Kasulu, Kahama, hivyo nitazungumza na wenzangu halafu nitasema nitagombea wapi,” alisema bila kutaja sababu za kutogombea jimboni kwake Kigoma Kaskazini.
Alisema kuhamia kwake ACT ni uamuzi sahihi kwa sababu chama hicho kinaendana na kile alichokuwa anakipigania kwa miaka yote.Aliongeza kuwa amehamia ACT si kwa bahati mbaya bali anajua nini anafanya na atahakikisha chama hicho kinakua na kuvipita baadhi ya vyama vya siasa vyenye umaarufu kwa sasa.