LILE sakata la mama kuwafungia ndani
watoto wake kwa miaka miaka 10 limechukua sura mpya baada ya mkuu wa
wilaya hiyo ya Mafia kwenda Kijiji cha Kanga na kumchukua mmoja wa
waliofungiwa, Muhadia Ally (pichani juu) ambaye hali yake bado ni mbaya
na kumpeleka hospitali ya wilaya.
Habari za mama mmoja kuwafungia ndani watoto wake zimeandikwa
mfululizo na gazeti hili kuanzia toleo namba 884 la Machi 31 na la
Aprili 7, mwaka huu na kumshitua Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Dk. Nassoro
Hamid aliyeamua kufunga safari hadi katika kijiji hicho akiwa
ameambatana na timu maalum ya watendaji wa wilaya.
Alikuwa ameongozana na ofisa wa dawati la jinsi kutoka jeshi la
polisi, ofisa ustawi wa jamii wilaya na ofisa mwandamizi kutoka ofisi ya
mkurugezi wa wilaya ya Mafia ambao majina yao hayakupatikana mara moja
kwa lengo la kuwachukua watoto hao na kuwapeleka hospitali.
“Nalipongeza gazeti la Uwazi kwa kufichua jambo hili na serikali itaangalia jinsi ya kuisaidia familia hii.
”Mimi mkuu wa wilaya nimepata taarifa hizi kupitia vyombo vya habari
yaani gazeti lako hivyo ninapongeza kazi mliyofanya, mmefanya kwa
umahiri mkubwa bila kuchoka,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Habari ambazo zimepatikana baadaye zinadai kuwa Mwasiti Ally ambaye
ni mama wa vijana hao kumbe mwanaume aliyezaanaye, Juma Mohamed yu hai
tofauti na alivyomsimulia mwandishi wetu kwamba alifariki dunia.
“Alifanya hivyo kwa kudhani kwamba akisema hana mume angesaidiwa kwa
haraka zaidi,” alisema mmoja wa majirani wa mama huyo na kwamba ni jambo
walilokuwa wamepanga.Watoto waliofungiwa ndani na mama huyo ni Mzee
Juma, Ally Juma aliyefariki dunia hivi karibuni na Muhadia Juma.Mkuu
huyo wa wilaya alisema kwa sasa Muhadia ameanzishiwa lishe maalumu huku
akipewa kila huduma inayohitajika.