Na Haruni Sanchawa
TUKIO
la aina yake! Dereva wa bodaboda aliyejulikana kwa jina la Alex Wilson
amekutwa ameuawa kwa kuchinjwa na kuporwa pikipiki lakini cha ajabu,
siku ya mazishi yake kaburini kukazikwa mgomba baada ya mwili kuzuiwa
usizikwe, Uwazi limechimba kisa kamili.
Ilikuwa Aprili 8, mwaka huu katika maeneo ya Mbezi Beach karibu na
Kiwanda cha Rafia, Alex ambaye ni mwenyeji wa Sumbawanga mkoani Rukwa,
aliuawa kwa kuchinjwa mfano wa kuku.Baada ya kifo hicho, madereva
bodaboda wenzake waliungana na kutafuta ndugu wa karibu ili kuwajulisha
kilichomkuta Alex.
Inadaiwa kuwa, katika kutafuta alikokuwa akiishi marehemu huyo,
wenzake walifanikiwa kupapata na kumkuta mtoto wa mama mwenye nyumba
ambapo walimuonesha picha za enzi za uhai wa Alex naye ndugu huyo
alikiri kwa kusema ni kaka yake.
Walimuuliza mtoto huyo aliko mama yake akasema yuko safarini Sumbawanga kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.
“Tulimwomba namba ya simu ya mama yake, akatupa. Tulipompigia alisema
kweli anamtambua marehemu lakini yeye yuko Sumbawanga,” alisema mmoja wa
madereva bodaboda hao.
Inadaiwa kuwa, bodaboda hao walimtaka mama huyo kutoa tamko juu ya
kuusafirisha mwili wa Alex kwenda Sumbawanga au kuuzika jijini Dar
ambapo alisema waende serikali ya mtaa kwa ajili ya kupata utaratibu
kisha wamzike.
“Siku iliyofuata, yaani Aprili 9, mwaka huu, tukiwa na baadhi ya
ndugu wa mbali wa Alex tulikwenda Kituo cha Polisi Afrikana (Dar)
kuomba kibali cha mazishi, lakini ikabidi polisi wafanye mawasiliano na
yule mama aliye Sumbawanga.
“Polisi walimpigia simu na kuweka loud speaker (spika kwa sauti ya
nje) wakimtaka mama huyo afike Dar haraka kwa mazishi ya mtoto wake au
waruhusu mtoto wake azikwe.“Lakini yule mama alijibu kuwa, wasijaribu
kufanya kitendo chochote cha mazishi kwa vile anajua kuwa mwanae huyo
hajafa na anajua alipo.
“Mama alisema watu wakifanya lolote watakiona maana yeye anatoka
Sumbawanga, hivyo zoezi la kuendelea na taratibu za maziko zikakwamia
hapo,” alisema bodaboda mmoja.Aliendelea kusema kuwa, wakati wanafanya
utaratibu wa kupata kibali tayari walishachimba kaburi kwa ajili ya
kumhifadhi marehemu. “Lakini baada ya mama kujibu vile, polisi
walifanya mawasiliano na viongozi wa juu na kuzuia maziko hadi ndugu
sahihi wapatikane na hivyo mwili wa maremu upo Hospitali ya Mwananyamala
(Dar) ukisubiri.”
Baada ya hapo bodaboda hao kwa kushirikiana na ndugu wa mbali,
walilazimika kukata mgomba na kuuzika kaburini badala ya mwili wa
marehemu.Mgomba huo ulizikwa katika Makaburi ya Kinzidi, Aprili 9, mwaka
huu kwa kile kilichodaiwa kuwa, kuacha kaburi wazi wakati
lilishachimbwa kwa ajili ya maziko ni uchuro kwa wengine walio hai.
Jumamosi iliyopita, Uwazi lilifanya jitihada na kumpata mama huyo kwa
njia ya simu ambapo alijitambulisha kwa jina la mama Dickson na kusema
yupo Mtaa wa Majengo wilayani Sumbawanga, Rukwa.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na marehemu Alex, mwanamke huyo alisema:
“Ni kweli Alex namfahamu na tulifahamiana Dar es Salaam na hii ni
kutokana na kunifahamu mimi ni mtu wa Sumbawanga hivyo siku za nyuma
alikuja nyumbani kwangu na kujitambulisha, mimi nilimchukulia kama
mwanangu.
“Ilifika mahali akawa ananiita shangazi, mahusiano yalikuwa ni
makubwa kutokana na kutoka sehemu mmoja yeye alinichukulia kama ndugu
yake wa karibu.“Mbali na kutoka sehemu mmoja sina undugu na Alex.”