Kama unadhani mipasho ipo katika nyimbo za taarabu tu, hakika utakuwa umekosea sana.
Hapa bungeni kauli zenye utata, kejeli na dhihaka ni mambo yaliyoshika hatamu tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti Mei 12.
Unajua ilikuwaje? Juzi usiku wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, waziri wa wizara hiyo Sofia Simba ni kama alijisahau kuwa yupo bungeni.
Mwanamama huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM (UWT) baada ya kubanwa na wabunge wa upinzani kuhusu suala la taasisi zisizo za kiserikali zilizosajiliwa chini ya wizara hiyo, aliwafananisha wabunge na upinzani na mtu ‘anayewashwa’.
Sijui bwana sababu ya waziri huyo kudai wabunge hao wanawashwa na sina hakika huko kuwashwa ni kwa aina gani ingawa yeye mwenyewe alidadavua baadaye kwamba hata akili ya mtu inaweza kuwasha.
Sitaki kunukuliwa vibaya bwana, kwani wewe mtu akikuambia unawashwa wakati hajakuona ukijikuna unadhani atakuwa anamaanisha nini?