Wednesday, May 27, 2015

Mwanamuziki Diamond Adaiwa Kuwatelekeza Watoto Shule..Akwama Kuwalipia Ada..Ni wale Walioshinda Kucheza Ngololo na Kuahidi Kuwasomesha

Gladness Mallya
KABANG! Staa anayevuna fedha nyingi kupitia kipaji chake cha muziki, Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amewatelekeza watoto katika Shule ya East Africa International jijini Dar ambao aliahidi kuwalipia ada, Risasi Mchanganyiko linakuwa la kwanza kukudondoshea.

Chanzo makini kililiambia gazeti hili juzi kwamba, baada ya Diamond kuwashindanisha watoto hao, Hillary na Hamis (katika picha no. 1 na 2 zilizoko ukurasa wa mbele walipelekwa shule na Diamond) katika shindano la Ngololo lililonyika Januari, mwaka jana katika Viwanja vya Leaders Club, Dar na kushinda aliamua kuwapeleka katika shule hiyo na kuahidi kuwalipia ada kila mwaka lakini kuanzia hapo aliwatelekeza.

“Jamani Diamond kila kukicha anafanya shoo za mamilioni lakini ameshindwa kuwalipia ada wale watoto ambao aliahidi kuwasomesha. Wamesoma mwaka mmoja tu,  mwezi uliopita walitimuliwa na sasa wako nyumbani. Inauma sana kwani hawa watoto walitolewa kwenye shule za kawaida na yeye ndiyo akawapeleka kule,” kilisema chanzo hicho.

WAZAZI WANASEMAJE?
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Fadhili alisema watoto wao walitimuliwa shuleni tangu April mwaka huu kwa kuwa, Diamond hakuwahi kuwalipia ada tangu alipowaingiza pale.“Inauma sana, kwani tangu watoto wetu watimuliwe tumekuwa tukifuatilia kwa mtu tuliyeambiwa ni msimamizi wa Diamond (jina lake linahifadhiwa kwa sasa) lakini hatupi jibu la kueleweka.

“Tulipewa namba za simu za mameneja wa Diamond, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ na Said Fella lakini kila tukiwapigia simu tunaambiwa msanii huyo hayupo Dar, mara amesafiri, mara yuko kwenye shoo, yaani kila siku tunazunguka tu hatujui tufanye nini.

“Tunaomba sana jamani, mtusaidie na nyie waandishi maana watoto wanapitwa na masomo na isitoshe kabla ya hapo walikuwa wakisoma kwenye shule za kawaida,” alisema mzazi huyo.

MSIKIE MWALIMU MKUU
Paparazi wetu alifunga safari mpaka shuleni hapo maeneo ya Mikocheni, Dar na kufanikiwa kuzungumza na Mwalimu Mkuu, Mercy Githirua ambapo alithibitisha watoto hao kusimamishwa masomo kutokana na kukosa ada.“Tulivumilia kwa muda mrefu sana kwani tulimwamini Diamond tukawapokea watoto hao na kuanza masomo. Siku aliyokuja kuwakabidhi hapa shuleni aliomba ‘invoice’ kwa ajili ya kututumia  ada lakini yuko kimya mpaka leo.

“Hata fedha ya kuwashonea sare za shule ilibidi niwasiliane na (linatajwa jina, linasitiriwa) maana tunafanya naye kazi nyingi, akatoa hizo fedha lakini ada ndiyo ikawa tatizo. Hivyo ilipofika Aprili 14, mwaka huu ilibidi niwarudishe nyumbani mpaka kieleweke kwa kweli.

“Sijapenda tabia ya Diamond, hivi anajua watoto wakimchukia itakuwa ni hatari sana kwake? Watoto wa watu walikuwa wanasoma huko akaenda kuwatoa na kuwaleta hapa lakini amewatelekeza, siyo vizuri kabisa,” alisema mwalimu mkuu huyo.

WANADAIWA SHILINGI NGAPI?
Kwa mujibu wa mwalimu mkuu huyo, watoto hao tangu walivyoingia Januari 21, 2014 hawakuwahi kulipiwa ada yoyote hivyo kila mmoja anadaiwa shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000).

DIAMOND, MAMENEJA WAKE!
Juzi, gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Diamond kwa njia ya simu lakini ilikuwa imesetiwa kwamba inafanya kazi muda wote ‘bize’ hata alipotumiwa meseji hakujibu. Vivyo hivyo kwa mameneja wake, Fella na Bab Tale simu zao ziliita bila kupokelewa.

TUJIKUMBUSHE
Mwaka jana, Diamond aliandaa shindano la Nani Anaweza Kucheza Staili ya Wimbo wa Ngololo ambapo watoto kibao walijitokeza Leaders Club. Watoto hao wawili waliibuka kidedea kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kucheza na ndipo zawadi yao aliamua kuwapeleka kwenye shule hiyo na kukutwa na yaliyowakuta!

GPL