MWISHO wa zama. Mwisho wa enzi. Kwa majonzi, kiungo mkongwe wa Barcelona, Xavi Hernandez ametangaza kuachana rasmi na klabu hiyo baada ya miaka 17 ya kucheza hapo na atakwenda kukipiga Al Sadd ya Qatar.
Juzi Alhamisi, Xavi 35, alitangaza mbele ya waandishi wa habari kuwa Barcelona ilikuwa imempa mkataba lakini akadai kwamba huu ulikuwa muda mwafaka kwake kuondoka katika klabu hiyo ambayo ameichezea tangu akiwa mtoto.
Mechi yake ya mwisho ya La Liga itakuwa leo Jumamosi dhidi ya Deportivo, kisha atacheza katika fainali za Kombe la Mfalme dhidi ya Athletic Bilbao halafu atacheza katika fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus Juni 6.
“Ni uamuzi sahihi, siyo rahisi sana, ni muda mwafaka wa kuondoka. Bado najiona nina matumizi sana hapa, lakini kubadilisha mazingira ni muhimu. Kichwa changu kinaniambia hivyo, ingawa moyo wangu hausemi hivyo,” alisema Xavi ambaye alidai lengo lake ni kumaliza masomo ya ukocha na kurudi Barcelona.
Aongoza mataji Hispania
Xavi alisainiwa na shule ya soka ya Barcelona mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 11. Tangu hapo ametwaa mataji 23 katika misimu 17 aliyocheza. Mpaka sasa amelingana kimataji na mkongwe wa Real Madrid, Francesco Gento ambaye pia ana mataji 23.
Kama akitwaa taji la Kombe la Mfalme dhidi ya Atletic, kisha akatwaa taji la Ulaya dhidi ya Juventus, Xavi atakuwa mchezaji mwenye mataji mengi zaidi katika historia ya Hispania. Xavi vilevile ameichezea timu ya Taifa ya Hispania mechi133.
Mastaa wafichua ya moyoni
Lionel Messi: “Ilikuwa raha sana kucheza na Xavi. Ni mchezaji anayefanya mambo yaonekane kuwa rahisi sana. Anaziona pasi ambazo ni yeye mwenyewe tu anayeziona.”
Sir Alex Ferguson (baada ya fainali za Ulaya 2009): “Messi hakuwa tatizo katika mechi hii. Tatizo lilikuwa kwa Iniesta na Xavi. Wangeweza kukaa na mpira usiku mzima.”
Pep Guardiola: “Xavi ni mchezaji mwenye vipimo vya damu ya Barcelona. Ana ladha na mpira. Mchezaji ambaye amebaki kuwa mpole na ni mzalendo na mwaminifu kwa klabu.”Johann Cruyff: “Kama Xavi ana siku mbaya, basi na Barcelona haitacheza mpira kama kawaida. Anatawala mechi na ndiye anayeamua mechi iwe vipi. Anacheza huku akiruhusu timu ifanye kazi. Ni mchezaji tofauti.”
Sandro Rosell (Rais wa Barcelona 2010-2014): “Tiki-taka (mpira wa pasi za haraka) ni utambulisho wa Xavi. Siku ambayo hatakuwa hapa, sidhani kama tutaendelea kucheza hivyo tena.”
Dani Alves: “Wakati tunaishi maisha ya leo, Xavi anaishi maisha ya baadaye. Anafikiria mbele ya kila mtu na anafanya mambo yawe rahisi sana.”
Vicente del Bosque: “Xavi amekuwa mchezji muhimu zaidi katika ubora wa miaka hii wa soka la Hispania. Ni vigumu kumwona mchezaji ambaye anaweza kuwa mbadala wake. Nafasi yake haizibiki.”
Sergio Busquets: “Ni mchezaji wa mfano kwangu na kwa wachezaji wote vijana wanaokuja na kujaribu kucheza katika kikosi cha kwanza.”
Iker Casillas: “Watu wananiuliza kila mwaka ni mchezaji gani wa Barcelona tungeweza kumchukua Real Madrid ili tuwe tunashinda? Kila mwaka jibu langu ni lilelile, Xavi. Uwezo wake wa kumiliki mpira na kuutumia mpira unamfanya awe mchezaji wao bora siku zote.”
Mechi yake ya kwanza
Bahati iliyoje. Mechi ya kwanza ya Xavi kwa Barcelona alicheza dhidi ya Manchester United katika pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika Uwanja wa Old Trafford Septemba 16, 1998. Alikuwa na umri wa miaka 18 na aliingia uwanja kipindi cha pili kocha akiwa Louis Van Gaal.
“Nakumbuka mechi yangu ya kwanza Old Trafford. Ilikuwa imeandaliwa vizuri, moja kati ya uwanja bora Ulaya na duniani. Niliingia uwanjani dakika chache baada ya Beckham kufunga bao la tatu kwa faulo. Baada ya hapo, Van Gaal aliniambia nipashe mwili moto,” anasema Xavi.
“Timu ilicheza vizuri kwa dakika zote 30 zilizobaki na niliondoka uwanjani nikijisikia vizuri sana kucheza mechi yangu ya kwanza,” alisema Xavi.