Mwanamke wa Kwanza ndani ya chama cha Mapinduzi (CCM) Amina Salum Ali, amevunja ukimya na kuamua kuweka wazi nia yake ya kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi oktoba.
Akizungumzia uamuzi huo, mwanasiasa huyo ambaye pia ni Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), amesema wanawake wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za juu za uongozi kwa kukosa fedha, lakini sasa ni wakati mwafaka kwao kujiamini katika jamii kwani uongozi siyo fedha bali ni uzalendo, kujikubali na kujiamini.
“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza kuifikisha nchi yangu katika uchumi wa kwanza kwa kutumia rasilimali zetu zikiwamo gesi, mafuta, kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu umefika kuwaongoza Watanzania.” amesema Amina
Amina aliwahi kushika nafasi za juu za uongozi Zanzibar na Tanzania Bara, ukiwamo uwaziri wa fedha Zanzibar.
Ameongeza kuwa wanawake wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia kugombea nafasi za juu za uongozi kwamba kunahitaji fedha hivyo wanaishia kuwa wanyonge."Siyo kweli, wajitokeze kwa wingi ili kitimiza ndoto za kuwajibika kwa taifa letu,” alisema.
Amina anaungana makada wengine wanaotajwa kuwania Urais mwaka huu ambao ni mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja , Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi , Teknolojia, January Makamba pamoja na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalah.