Wednesday, May 27, 2015

Yanga SC yamleta Samatta Dar

Mbwana Samatta.
Wilbert Molandi,Dar es Salaam
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wanatarajiwa kuwaleta mabingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), Kaizer Chiefs, pamoja na TP Mazembe wanaocheza Watanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kwa ajili ya kuwapima nyota wao wapya waliowasajili.
Yanga hadi sasa wamefanikiwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Deus Kaseke huku ikiwabakiza Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao ilikuwa ikidaiwa kuwa wanaweza kutimka.
Timu hiyo, bado inaendelea na usajili na hivi sasa inawania saini ya mshambuliaji wa Platinum FC ya Zimbabwe, Donald Ngoma, Haruna Chanongo wa Simba na Salum Mbonde wa Mtibwa Sugar.
Akizungumza na Championi Jumatano, ofisa habari wa timu hiyo, Jerry Muro, alisema kuwa wamepeleka barua za mialiko kwenye klabu mbalimbali zitakazofika kusherehekea sherehe yao ya ‘Yanga Day’ itakayofanyika Juni 15, mwaka huu.
Muro alisema, tofauti na Kaizer Chiefs wamezialika Zesco ya Zambia na TP Mazembe ya akina Samatta.
Aliongeza kuwa kwa upande wao siku hiyo ya sherehe wamepanga wacheze na Kaizer Chiefs huku TP Mazembe na Zesco zikipambana zenyewe.
“Tumepanga sherehe maalum kwa ajili ya mashabiki wa Yanga ambayo ni Juni 15, mwaka huu ambazo shughuli hizo zitaendana na sherehe ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara tuliouchukua.
“Katika kusherehekea sherehe hizo, tumezialika klabu kubwa mbalimbali kutoka nje ya nchi zitakazofika kusherehekea pamoja na kucheza mechi.
“Tumeialika Kaizer Chiefs tutakayocheza nayo mechi siku hiyo kwa ajili ya kuwapima na kuwatambulisha wachezaji wetu wote tuliowasajili tutakaowatumia msimu ujao wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.
“Pia tumewaalika TP Mazembe na Zesco ya Zambia watakaocheza mechi yao ya utangulizi, kiukweli tumepanga kufanya bonge la ‘bash’ siku hiyo.
“Nafikiri kila mmoja anajua kuwa Samatta na Ulimwengu ni wachezaji mahiri sana hapa nchini, hivyo watakuwepo nao kunogesha sherehe hiyo,” alisema Muro.