Maajabu ya Bagamoyo! Katika hali ya kushtua, familia yenye makazi yake, Magomeni, Bagamoyo mkoani Pwani, imejikuta kwenye mauzauza baada ya ndugu yao kufariki dunia huku akidaiwa kukohoa, kufumbua macho na kuonesha dalili za kuwa hai, pamoja na kwamba daktari alithibitisha kifo.
WAOMBOLEZAJI WATIMUA
Katika tukio hilo lililosababisha waombolezaji kutimua mbio lililojiri Juni 28, mwaka huu, binti wa familia hiyo, Tunu Shabani (36), alifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kutokana na kuumwa kichwa ghafla.
MUME ASIMULIA
Akizungumza na Amani lililofunga safari kutoka Dar hadi Bagamoyo, mume wa Tunu, Iddi Ramadhani alisema mkewe alianza kupata maumivu ya sikio baadaye kichwani ambapo alimhamishia kwa wazazi wake maeneo hayohayo ya Magomeni kwa kuwa ni karibu na hospitali.
Iddi alisimulia kuwa Juni 27, mkewe huyo alipelekwa kwenye hospitali hiyo, akatundikiwa dripu lakini hali ilizidi kuwa mbaya kiasi cha kuwekewa mashine ya kupumulia kabla ya kuaga dunia alfajiri ya Juni 28.
“Baada ya daktari kuthibitisha kifo cha mke wangu, ndugu tulikutana, tukaandaa mazishi kwa kuchimba kaburi na shughuli ya kuandaa maiti kwa ajili ya mazishi tuliyopanga yafanyike saa 6:00 siku ya pili yake yaani Juni 29.
“Wakati wa kuosha maiti mara tukasikia sauti kasha ikafumbua macho, miguu yake ikajinyoosha na mwili ukawa na joto.
“Ilibidi tusitishe kumzika kwanza na kujaribu kumtafuta daktari,” alisema Idd.
Aliongeza kuwa, hali ya marehemu iliendelea kuwatatiza kwa kuwa wataalam walishindwa kufanya chochote hadi Juni 29, walishangazwa zaidi kuona maiti ikiwa inatoka jasho jingi huku joto likiendelea kuwa vilevile.
SHEHE ANENA
Akizungumza na waandishi wetu, shehe aliyekuwa akisimamia kuandaa maiti, Mtawa Adam (pichani) alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu za mazishi za Dini ya Kiislam, marehemu ambaye ni mwanamke huoshwa na wanawake wenzake, kanuni ambayo mwili wa Tunu nao uliipitia.
Shehe Adam alisema kuwa, kama kawaida alimpima marehemu na kumshonea sanda huku akisubiria wanawake hao wamalize kumuosha na kumuandaa ili yeye aingie kwa ajili ya kumnyosha viungo, lakini kabla hawajamaliza, alishtushwa kuwaona wakitoka mbio na kudai maiti imefumbua macho na kunyoosha mguu.
“Niliingia ndani na kumuona marehemu ambapo wakati huo alikuwa amefumba macho, nilipomgusa alionekana wa moto kama alikuwa hai, nikamtazama nyayo zake zilionekana ni nyeupe tofauti na za marehemu ambazo huwa za njano.
“Nilimrekebisha mguu wake aliounyoosha, lakini nikashangaa ukirudi tena kama ulivyokuwa awali na hata mapigo yake ya moyo yalikuwa yakipiga mara moja baada ya dakika hata mbili,” alisema shehe huyo na kuongeza kuwa aliwashauri wanafamilia wamuondoe Tunu kwenye kitanda cha maiti na kughairi maziko huku daktari mwingine akiitwa kumpima lakini naye alisema alifariki dunia.
UMATI WAJAA
Waandishi wetu, walishuhudia umati wa waombolezaji wakiwa wamezunguka eneo hilo ili kushuhudia kilichoendelea.
MAMA APANDISHA MASHETANI
Katika hali isiyo ya kawaida, mama mmoja alipandisha mashetani na kudai Tunu hajafa.
WAGANGA WANNE
Kwa mujibu wa ndugu mmoja wa familia hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, waliwaita waganga wa nne wa kienyeji ambapo mmoja alifika na kudai Tunu alichukuliwa msukule lakini alishindwa kumfanya awe hai.
Aidha, waganga waliobakia licha ya kufanya ndumba zao, Tunu hakuweza kuamka kama walivyodai awali.
Baba mzazi wa marehemu, Adam Hassan akizungumza na waandishi wetu alisema Tunu hakuonesha dalili za kuwa hai hivyo taratibu za mazishi zilifanyika kesho yake (Juni 30) na kuzikwa katika Makaburi ya Kiwangwa, Bagamoyo.