Tuesday, September 15, 2015

Mtoto aibwa na punda, ushirikina watajwa

mntoto-(2)Mtoto anayedaiwa kuibwa na punda.
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Tukio ambalo si la kawaida limetokea Kahama mkoani Shinyanga ambapo mtoto wa miezi mitano aliibwa na punda na kuzua tafrani kubwa.
Purukushani hiyo ilitokana na punda huyo kumng’ata na kuanza kukimbia naye mtoto katika Soko la Lumambo wilayani Kahama.
donkeyMfano wa punda aliyeiba mtoto
Akizungumza na mwandishi wetu katika wodi ya watoto Hospitali ya Wilaya ya Kahama, mama mzazi wa mtoto huyo, Dafroza John (23), mkazi wa Mtaa wa Shunu wilayani hapa alisema mwanaye alichukuliwa na punda huyo alipokuwa amemweka chini wakati yeye akiwahudumia wateja chakula katika soko hilo.
Mwanamke huyo huku akiwa amemshikilia mwanaye hospitalini hapo, aliongeza kuwa baada ya mwanaye kuchukuliwa na punda huyo alianza kupiga kelele za kuomba msaada na ndipo wasamaria wema wakajitokeza na kumfukuza kwa umbali wa zaidi ya mita 100 hadi alipomwachia na kukimbia.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Sudi Thomas aliliambia gazeti hili kuwa, walimkimbiza mnyama huyo, wengine wakiwa na bodaboda, wengine kwa baiskeli na wengine kwa miguu kisha mtu mmoja aliyemfikia akampiga kwenye shingo na fimbo ndipo akamwachia mtoto huyo.
mntoto (1)Mama mzazi wa mtoto huyo, Dafroza John
Hata hivyo, licha ya  punda huyo kusalimu amri na kukimbia, wasamaria wema hao waliamua kumkimbiza hadi walipomkamata na kisha kuanza kumshambulia kwa mawe hadi kumuua na kumchoma moto.
Muuguzi wa zamu katika wodi ya watoto katika hospitali hiyo,  Bundala Boniface alisema mtoto huyo amepata majeraha sehemu ya kifua na bado wanaendelea kumpatia matibabu.
Hili ni tukio la kwanza la aina yake ambalo limezua maswali miongoni mwa wakazi wa Kahama kwa punda kumwiba mtoto kwa mdomo na kukimbia naye ambapo baadhi ya watu wamehusisha tukio hilo na ushirikina.
“Ni jambo la ajabu, punda ni rafiki wa binadamu, iweje akimbie na mtoto? Kwanza punda hali nyama, iweje amchukue mtoto?” alihoji mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Asha Bakari, mkazi wa Kahama.