Banda alionyeshwa kadi mbili za njano na refa wa Bukoba, Jonesia Rukyaa ndani ya dakika nne kwa kumchezea rafu Donald Ngoma mara zote na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 24 katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na ikiwa pungufu, Simba SC ilipachikwa bao la kwanza dakika ya 39, mfungaji Donald Ngoma – kabla ya Amissi Tambwe kufunga la pili dakika ya 72.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mayanja alisema kadi nyekundu aliyoonyeshwa Banda ndiyo iliyowagharimu hadi kupoteza mchezo.
Kocha wa Simba SC, Mganda Jackson Mayanja (kushoto) amesema kutolewa kwa Abdi Banda kuliigharimu timu yake kufungwa 2-0 na Yanga |
“Tulicheza vizuri sana dakika 20 za mwanzo, lakini baada ya kadi ilibidi tubadili mfumo na wenzetu wakatumia nafasi hiyo kutushinda” alisema Mayanja.
Simba jana imefungwa 2-0 na Yanga katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Donald Dombo Ngoma kipindi cha kwanza na Amissi Joselyn Tambwe kipindi cha pili.
Matokeo hayo yanaishusha Simba kutoka kileleni hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, ikibaki na pointi zake 45 baada ya kucheza mechi 20, wakati Yanga iliyofikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 19 inapanda kileleni, huku Azam FC ikisogea nafasi ya pili baada ya kuifunga Mbeya City 3-0 mjini Mbeya na kugikisha pointi 45.
Simba SC jana ilipata pigo mapema tu dakika ya 24, baada ya beki wake wa kati, Abdi Banda kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Jonesia Rukyaa wa Kagera kwa kumchezea rafu Ngoma.
Mshambuliaji wa Zimbabwe, Ngoma akaifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 39, akitumia makosa ya beki wa kulia wa Simba SC, Hassan Kessy aliyemrudishia pasi fupi kipa wake Vincent Angban raia wa Ivory Coast.
Ngoma aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC, baada ya kusajiliwa kutoka Platinum FC ya kwao, aliiwahi pasi ya Kessy kabla haijamfikia Angban na kumlamba chenga kipa kisha kufunga.
Krosi maridadi ya winga Godfrey Mwashiuya kutoka upande wa kushoto iliunganishwa nyavuni kwa guu la kulia na Mrundi Tambwe dakika ya 72 kuipatia Yanga SC bao la pili.