RAIA wa Pakistan,
Kamran Ahmed, aliyetuhumiwa na kisha kutiwa hatiani katika kashfa ya kutorosha
wanyamapori hai 130 wa aina 14 tofauti, alikuwa na vibali vyote halali kutoka
serikalini, Raia Mwema linaweza kuthibitisha.
Mpakistan huyo
alitoweka akiwa chini ya dhamana, akahukumiwa bila kuwapo mahakani na sasa
imedhihirika kwamba kutoweka kwake kulikuwa ni kuficha ushiriki wa vigogo
katika mpango wa kuuziana wanyama hao.
Uchunguzi wa muda
mrefu wa Raia Mwema, umebaini kwamba Kamran Ahmed alikuwa na vibali vyote
muhimu vya kusafirisha wanyama hao pamoja na hati ya makubaliano (MoU), kati
yake na Idara ya Wanyamapori ya Tanzania.
Wanyama hao hai wenye
thamani ya shilingi milioni 170 za Tanzania walisafirishwa Novemba 26, 2011,
kwa Ndege ya Jeshi la Qatar (Emir Air force) kupitia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Hati ya makubaliano
(MoU) ambayo Raia Mwema inayo nakala yake, inaonyesha kuwa kulikuwa na
makubaliano kimaandishi baina ya Kamran, kama Wakala wa Halmashauri ya Jiji la
Karachi nchini Pakistan (CDGK) na Erasmus Tarimo, kama mwakilishi wa Serikali
ya Tanzania.
Tarimo alikuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori kati ya mwaka 2007 na 2011, kabla ya
kustaafu kwa mujibu wa sheria. Alitia saini hati hiyo Mei 28, 2009 kwa niaba ya
Wizara ya Maliasili na Utalii.
Aidha, imebainika kuwa
kabla kutiwa saini makubaliano hayo, ofisa wa Serikali ya Tanzania
aliyetambulika kwa jina moja la Midele alikwenda Karachi-Pakistan kukagua
bustani ya kutunzia wanyama (zoo) ambako wangepelekwa wanyama hao kutoka
Tanzania.
Kwa mujibu wa picha
zilizopatikana kutoka vyanzo vya uhakika vya habari vya gazeti hili, Midele
anaonekana akiwa mbele ya lango la kuingilia katika bustani wakati nyingine
zinamwonyesha akiwa na maofisa kadhaa wa Serikali ya Pakistan katika “miondoko”
tofauti.
Taarifa zinadai kuwa
Midele alikwenda Pakistan kwa kulipwa gharama zote na Kamran, ikiwa ni pamoja
na posho za kujikimu, nauli ya ndege na gharama ya malazi. Baada ziara hiyo,
hati hiyo ya makubaliano ndipo ilipotiwa saini.
Hati hiyo yenye kurasa
nne ina vipengele 16 na imeainisha kuwa wanyama watakaokamatwa na kusafirishwa
hawatatumika kwa shughuli za kibiashara.
“Malengo ya Hati (MoU)
hii ni kujulisha ridhaa ya Wizara ya Malialisili na Utalii kuipatia Halmashauri
ya Jiji la Karachi nchini Pakistan (CDGK) tembo watoto wanne (4), kwa ajili ya
Zoo (bustani ya kuhifadhia wanyama) ya Karachi na hifadhi, kwa madhumuni ya
kutoa elimu na uhifadhi,” inasema sehemu ya kwanza ya hati hiyo.
Hata hivyo,
haikufahamika mara moja iwapo bustani ya wanyama ya Karachi ni ya kibiashara au
kwa ajili ya huduma za kijamii.
Nyaraka zaidi
zinabainisha kuwa katika kashfa hiyo, maofisa wa Idara ya Wanyamapori Tanzania
ndiyo waliohusika kuwakamata twiga hao na wanyama hai wengine, wakilipwa posho
na Kamran.
Aidha, pia vitendo
hivyo vimefanyika kinyume cha Sheria ya Tanzania ya Wanyamapori (Wildlife
Conservation Act) ya mwaka 2009, ambayo inazuia biashara ya wanyamapori hai.
Sura ya 5 kifungu cha
(2) kipengele (a) (b) na (c) kinafafanua kuwa mtu au taasisi itaruhusiwa
kukamata mnyama wa aina yoyote kwa sababu tu za utafiti, elimu, kiutamaduni na
si kwa sababu za kibiashara.
Uchunguzi unaonyesha
kuwa katika kipindi chote wakati biashara hiyo ikifanyika nyaraka za serikali
zilitumika tu kwa malengo ya kujikinga na mkono wa sheria pale mambo
yatakapoharibika.
Kwa mujibu wa vyanzo
kadhaa vya habari, Kamran alikuwa anawalipa maofisa wote wa serikali
waliofanikisha mipango hiyo kwa fedha za kigeni kati ya dola za Marekani 20,000
na 50,000 kama “huduma ya kuwanunua” wanyama hao.
“Katika kipindi cha
miaka miwili kabla ya kufichuliwa kwa kashfa hiyo maafisa wa Idara ya Wanyapori
walipokea fedha kutoka kwa Kamran kama rushwa na wao walimtengenezea nyaraka za
kiserikali ili wanyama wafike salama huko sokoni,” anadai mmoja wa watu wa
karibu wa Kamran.
Kwa mujibu msiri huyo,
Kamran alikuwa na mtandao mpana wa usafirishaji wanyama hai duniani kiasi cha
kuwekwa katika orodha maharamia 139 waliokuwa wanatafutwa na Polisi wa
Kimataifa (Interpol) katika nchi 36 dunia kote.
Operesheni ya
kuwatafuta watu hao ilipewa jina la “infra terra” na ilizinduliwa Oktoba mwaka
2014 na Kamran alikuwa mtu wa 17 katika orodha hiyo.
Mtandao wa Kimataifa
wa Interpol unamtaja Kamran kuwa ni raia wa Pakistani, aliyezaliwa mwaka 1985,
anatafutwa na Serikali ya Tanzania kwa kosa la kusafirisha wanyama hai kutoka
Tanzania kwenda Qatar. Interpol wanaeleza kuwa Kamran alilipa gharama za
usafiri wa ndege ya kijeshi iliyopakia twiga na swala kutoka Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda Qatar.
Kwa mujibu wa Mfuko wa
Wanyamapori Duniani (World Wildlife Fund - WWF), utoroshaji wa wanyama hai ni
biashara kubwa inayoendeshwa na mtandao hatari wa kimataifa.
Mtandao
huo husafirisha wanyama hai na viungo vya wanyama kama ilivyo kwa dawa za
kulevya na silaha.
Kutokana na jinsi
biashara hiyo inavyoendeshwa, mfuko huo unakiri kuwa ni vigumu kujua kwa
uhakika gharama halisi ya biashara hiyo haramu.
Lakini wataalamu
mbalimbali wanakadiria thamani ya biashara hiyo kuwa Dola za Kimarekani bilioni
20, na kuifanya kuwa ni biashara haramu ya nne inayoingiza pesa nyingi duniani,
ikitanguliwa na dawa za kulevya, noti bandia na usafirishaji wa binadamu.
Source: Raia Mwema
