Chuchu Hans Mayasa Mariwata,RISASI Mchanganyiko
DAR ES SALAAM: Habari mpya mjini kwa sasa ni kuwa wale mahasimu wawili wa muda mrefu, Blandina Chagula ‘Johari’ na Chuchu Hans ambao ni mastaa wenye majina makubwa katika kiwanda cha filamu nchini, wamemaliza tofauti zao na sasa ni mashostito wakubwa, Risasi Mchanganyiko lina ubuyu mzima.
Chanzo cha kuaminika kililiambia gazeti hili kuwa, mabinti hao ambao sababu ya bifu lao linatajwa ni kumgombea kimapenzi Vincent Kigosi ‘Ray’ ambaye pia ni muigizaji, hivi karibuni walionekana wakiwa wamekaa pamoja katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam na wakati mwingine wakiitana chemba walipozungukwa na watu.
“Niaje mdaku? Ninakumegea ubuyu kwamba Johari na Chuchu hivi sasa ni mashosti ile mbaya, kwa macho yangu nimewaona pale Leaders wakibadilishana mawazo, tukapigwa na bumbuwazi. Tumeambiwa kuwa kazi yote hiyo imefanywa na Steve Nyerere,” chanzo chetu kilitiririka.
Baada ya kuunyaka ubuyu huo, gazeti hili lilianza na Chuchu ambaye simu yake iliita bila kupokelewa, lakini kwa upande wake Johari alipotakiwa kuidadavua ishu hiyo, aliishia kucheka na kudai hataki kuongelea mambo hayo.
“Mmh jamani nani kakwambia hiyo habari, mmeshaanza mambo yenu, mimi sitaki kuongelea hizo ishu, achana nazo bwana,” alisema Johari huku akiangua kicheko.
Ili kuweka mambo sawa, Steve Nyerere, Mwenyekiti wa zamani wa Bongo Muvi alipatikana kupitia simu yake ya mkononi;
“Ni kweli hawa wasanii hivi sasa wamemaliza tofauti zao, kwani wewe huoni kama hili ni suala la heri au hukutaka wapatane? Hiki ni kitu cha kumshukuru Mungu. Kuhusu kuwapatanisha hilo mimi sijui, ila wewe elewa tu kuwa hivi sasa wanaelewana mno.”
Awali, Johari alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ray, uliosababisha wawili hao kuanzisha kampuni yao inayojishughulisha na mambo ya filamu ya RJ Company, lakini ghafla Chuchu Hans alianza kuonekana akiwa na ukaribu na mwanaume huyo, kitendo kilichosababisha kuwepo na kutokuelewana kati yao kulikodumu kwa muda mrefu.