Hatimaye uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam umekamilika leo katika ukumbi wa Karimjee, na kushuhudia Isaya Mwita wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Mwita ameibuka na ushindi na kutangazwa kuwa Meya Mpya wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kupata kura 84 akimshinda mpinzani wake, Yenga Omary wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 67.
Uchaguzi huo umeweka historia ambapo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi (1992), Chama Cha Upinzani kimepata nafasi ya kuongoza jiji hilo.
Uchaguzi huo uliahirishwa mara kadhaa kutokana na mvutano uliokuwa unaibuka kati ya wajumbe wa CCM na Chadema na kuzua vurugu wakati mwingine.