Thursday, March 24, 2016

Wa kumtoa Babu Seya huyu hapa

øøNguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha wakiwa mahakamani.
Waandishi wetu, amani
DAR ES SALAAM: Jaji wa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCPHR) yenye makao makuu yake jijini Arusha anayesimamia rufaa ya kesi ya Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ (pichani), Dk. Robert Eno raia wa Cameroun, amelieleza Amani kinachoendelea kwenye kesi hiyo.
Katika mahojiano maalum na gazeti hili kwa njia ya simu yaliyochukua takriban dakika kumi Jumatatu wiki hii,  jaji huyo alisema bado kesi hiyo inaendelea lakini kila kitu kitafikia ukomo Mei, mwaka huu.
MSIKIE MWENYEWE
“Ni kweli bado kesi hiyo ipo kwenye usimamizi wa mahakama hii na mimi ndiye Jaji Msajili wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu hivyo hujakosea. Pia ni kweli ipo chini yangu,” alisema jaji huyo kwa sauti yenye ushirikiano mkubwa.
Akaendelea: “Kesi ilikuwa ikiendelea kwenye mahakama ya siri (chamber court).
“Lakini tumeshaiandikia Serikali ya Tanzania maombi ya kuruhusu kusikiliza publically (kwa uwazi), bado hawajatujibu lakini watatujibu ndani ya muda mfupi. Nina uhakika kila kitu kitakuwa tayari na Mei ndipo itajulikana.”
Babu-Seya-na-mwanaye-papii...Wakiwapungia mashabiki wao.
ITAKAVYOKUWA
Jaji Eno akaendelea kusema: “Kinachofanyika sasa ni kwamba baada ya serikali kutujibu, tutakaa kama kamisheni ya haki za binadamu Afrika kujua namna ya kuiendesha kesi hiyo.”
KABLA YA JAJI
Awali kabla ya kuzungumza na Jaji Eno, Amani lilizungumza na mmoja wa makatibu muhtasi ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji wa mahakama hiyo ambaye alieleza kuwa kesi hiyo yenye namba 38/006/2015 ilifunguliwa Februari 11, 2015 ikipewa jina la Nguza Viking and Another na kwamba aliyekabidhiwa faili lake ni Jaji Eno hivyo ndiye anayeweza kuitolea ufafanuzi.
LENGO LA GAZETI LA AMANI
Awali kesi hiyo ya rufaa ilikuwa itolewe maamuzi Machi 11, mwaka huu lakini ukapita ukimya hivyo kulifanya Amani kumtafuta rais wa mahakama hiyo, Jaji Augustine Ramadhan na ndipo simu ikatua mikononi mwa katibu muhtasi huyo.
Katibu: “Haloo.”
Amani: “Naongea kutoka Gazeti la Amani la Global Publishers. Nataka kuzungumza na Jaji Augustine Ramadhan.”
Katibu: “Kwa shida gani?”
Amani: “Nataka kujua rufaa ya Babu Seya na Papii Kocha ilipoishia.”
Katibu: “Huku ni Nguza Viking na mwingine. Sasa Jaji Augustine ni mbali sana. Kuna jaji anaitwa Dk. Robert Eno. Katoka, akija nitakuunganisha naye. Ni raia wa Cameroun.”
SEYA….Wakifuatilia jambo.
NCHINI TANZANIA
Wakati Jaji Eno akitoa tamko hilo, nchini Tanzania habari zinasema kuwa familia ya wanamuziki hao sasa inakesha kwenye maombi ili kuhakikisha hukumu dhidi ya rufaa hiyo inawatoa jela wafungwa hao.
Mmoja wa wanafamilia ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema: “Safari hii nyota iko kwao. Wamekaa sana gerezani sasa Mungu amewaona. Tunaamini mahakama itajua kuwa haki ya wafungwa wake ni kutoka na si kuwa jela.”
WAKITOKA WATAFIKA GLOBAL PUBLISHERS
Baada ya kuzungumza na mwanafamilia huyo, Amani lilizungumza na mtoto wa kwanza wa Nguza, Mbangu ambapo alisema:
“Nilishasema kuna watu nimewaachia kushughulikia rufaa ya mzee na bwana mdogo (Papii). Kama ishu ni kutoka mimi simtazamii jaji, imani yangu ipo kwingine kabisa.
“Nakuahidi watatoka na wakitoka lazima nitawaleta hapo Global Publishers, mtawaona wala msiwe na shaka. Kutoka ni lazima si kwa jaji, ila kwa Mungu wangu.”
WANACHOKIDAI AKINA NGUZA
Kupitia shauri lao lililowasilishwa mahakamani na jalada lake kupewa namba 006/ 2015, wanaiomba Mahakama ya Afrika kutoa uamuzi kuwa haki zao zilivunjwa na wanaomba waachiwe huru na kulipwa fidia.
Pia wanataka mahakama hiyo iteue wataalamu watakaotoa ufafanuzi wa hoja za kesi yao na kuisaidia kufikia wajibu wake.
Miongoni mwa hoja za Babu Seya na mwanaye zilizosikilizwa mahakamani hapo ni pamoja na kwamba mwenendo wa shauri lao haukufanyika kwa kuzingatia haki, vilevile wanadai hati ya mashtaka dhidi yao ilikosewa kuandikwa tarehe ambayo tuhuma za makosa yao zilidaiwa kufanywa hivyo wakashindwa   kutayarisha utetezi wao.
Pia  wanadai  mahakama iliyowatia hatiani ilijielekeza katika  ushahidi wa upande wa mashtaka pekee usioshirikisha ushahidi mwingine……Wanadai Serikali ya Tanzania kupitia maofisa wake, ilivunja misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa kwani ilivunja Ibara 1, 2, 3, 5, 7(1)b), 13 na 18(1) ya Mkataba wa Afrika kuhusu Ubinadamu na Haki za Binadamu.
Malalamiko mengine ni kuwa baada ya kukamatwa hawakuelezwa mapema kuhusu mashtaka waliyokuwa wakituhumiwa nayo na  waliwekwa chini ya ulinzi kwa siku nne bila kuwa na mawasiliano na kupata fursa ya kuonana na mwanasheria au mtu mwingine yeyote.
WANADAI WALITESWA
Wanadai wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, waliteswa na kutukanwa na baadaye ofisa mmoja wa polisi aliwaeleza kuwa wanatuhumiwa kwa ubakaji.
WALISINGIZIWA
Wanadai kwamba mashtaka dhidi yao yalitungwa na hivyo hukumu iliyotolewa haikujikita katika ushahidi wenye nguvu katika sheria.
TUMEFIKAJE HAPA?
Nguza na wanaye watatu walikamatwa Oktoba 12, 2003 na kufikishwa Kituo cha Polisi  Magomeni, Dar, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Oktoba 16, 2003 wakituhumiwa kubaka na kunajisi watoto 10.
Baada ya kusikilizwa kesi hiyo, Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, Addy Lyamuya  aliwatia hatiani Babu Seya na wanaye kwenda jela maisha.
Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu.
Awali mwaka 2004, baada ya kukutwa na hatia katika kesi hiyo, Babu Seya, Papii Kocha na wakili wao, Mabere Marando walikata rufaa ya pili ambayo ilitupiliwa mbali.
Mwaka 2010 waliomba tena rufaa ambayo marejeo yake yalisikilizwa na kutolewa hukumu Februari, 2010. Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha, ikawaachia huru watoto wake, Nguza Mbangu na Francis Nguza.
GPL