Friday, October 10, 2014

SHUGHULI ZA KIJAMII ZAMFANYA RAY C KUWEKA MUZIKI PEMBENI KWA MUDA

Msanii wa muziki nchini, Rehema Chalamila aka Ray C ambaye pia alianzisha taasisi ya kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya, ‘Ray C Foundation’, asema kazi ya kuwaokoa vijana walioingia kwenye dibwi la matumizi ya madawa hayo imemfanya auweke muziki pembeni. 

Ray C ameiambia Bongo5 kuwa tangu January mwaka huu alikuwa na mpango wa kuachia kazi yake mpya lakini majukumu ya kijamii yamemzuia kufanya hivyo. 

“Baada ya Fiesta mwezi wa kumi na moja ntatoa wimbo wangu wa kwanza, itasikika kwa mashabiki wote ambao wananisubiria. Ilitakiwa itoke tangu mwezi wa kwanza ila kutokana na mimi moyo wangu kuwepo kwenye kusaidia jamii nikasema ngoja nisubiri kidogo muziki niweke pembeni nisaidie vijana wenzangu nao watoke kwenye madawa, kwasababu ni bahati nimekuwa hai. Nikasema kama Mungu ameniokoa basi na mimi nisaidie wengine ambao wana matatizo na muziki niweke pembeni kwasababu muziki hauna umri. Muziki mpaka uzee nitafanya lakini nikaona niweke pembeni kidogo.” 

“Namshukuru Mungu response ya foundation yetu imekuwa nzuri sana, watu wanaingolea vizuri na tumeshasaidia vijana zaidi ya 50 kuingia kwenye tiba. Tumeshaajiri vijana kibao na kua mradi pia wa Ray C Foundation kupitia mradi wetu wa Mmgahawa ambao tumeajiri waathirika ambao wameamua kuachana na madawa ya kulevya ambao wanaendelea vizuri. Kwahiyo naona sasa hivi nimekuwa super hata nikirudi kwenye muziki kidogo nikitoa wimbo na foundation nikiipekeka kwa pamoja itakuwa vizuri,” amesema Ray C. 

Ray C ameongeza kuwa taasisi yake inafikiria kufanya harambee mapema mwakani ili kuongeza uchumi wa tasisi hiyo ambayo kwa sasa inajiendesha yenyewe bila msaada wowote. 

“Kwa sasa hivi tumeanza hapa Dar es Salaam lakini tunatarajia kufungua branch tofauti tofauti mikoa yote kwaajili ya kusaidia waathirika ambao wako mikoani huko kuweza kutoka kwenye madawa na kupata elimu ya kutosha ili waweze kuepukana na madawa ya kulevya,” ameeleza. “Changamoto kubwa sisi ni wafadhili, bado hatujaanza kupata wafadhili rasmi. Sasa hivi unavyoona kila kitu nachofanya kupitia foundation yangu ni kupitia mfukoni kwangu, sijapata mdhamini yoyote. Kwahiyo far tunataka kama mwaka kesho kama mwezi wa pili tutajaribu kufanya utaratibu wa kuyaalika makampuni mbalimbali na kufanya harambee kuchangia mfuko wetu ili kuwavuta vijana wengi zaidi ambao wameathirika na madawa wa kulevya. Kama mikoani ni lazima tusafiri, tuwasaidie watu nauli ili wengine waweze kufika Dar ili waweze kupata tiba na baada ya hapo kuwasimamia ili wapate ajira ili waweze kumudu mahitaji ya kawaida kwanza. Kwa sababu wengi ambao wanaacha madawa ya kulevya wakirudi katika mazingira magumu wanakaa na wanaweza kupotea tena. Ni lazima tuwatengezee mazingira mazuri.”