Pichani kulia ni picha ya mjusi iliyowekwa kwenye ukurasa wa mbele wa tovuti ya Shirika la Ndege la Malaysia.
WADUKUZI wa mitandao wameweka picha ya mjusi na wimbo katika tovuti ya Shirika la Ndege la Malaysia ambamo wameweka ujumbe usemao kwamba ‘Ndege Haipatikani’ ukihusishwa na ndege namba MH370 ya shirika hilo ambayo ilipotea mwaka jana mwezi Machi na haijapatikana mpaka leo.
Wadukuzi hao ambao wanajiita Lizard Squad wameivamia tovuti hiyo ya www.malaysiaairlines.com na kuweka picha ya mjusi huyo ambaye amevaa kofia akiwa na kiko na koti maalum litumikalo kwenye milo ya jioni. Picha hiyo iliambatana na wimbo maalum wa ‘rap’.
Katika taarifa yake, shirika la Malaysia Airlines lilikiri kwamba tovuti yake imevamiwa na watumiaji wake walikuwa wakielekezwa kwenye tovuti ya wadukuzi hao.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa tatizo litakuwa limetatuliwa ndani ya saa 22.