Monday, February 2, 2015

HII SI SAWA! SHEHENA ZA MADAWA ZAHARIBIKA HOSPITALI, ZATUPWA JALALANI

WAKATI wagonjwa wakifa kwa kukosa dawa hata kidonge kimoja kwenye hospitali mbalimbali nchini, katika hali ya kushangaza, shehena kubwa ya madawa katika Hospitali Rufaa ya Morogoro imeteketezwa kwa moto baada ya kuharibika kwa kupita muda wake wa matumizi, Ijumaa Wikienda linakuwa la kwanza kukujuza.
Madawa ya hospitali yakishushwa kwenye gari ili kuteketezwa.
Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni mjini hapa ambapo paparazi wetu alitonywa kuhusiana na kuwepo kwa ishu hiyo ambapo alikwenda na kushuhudia lori lenye uzito wa tani 7 likisomba dawa hizo zilizoharibika kwa awamu nne mfululizo na kwenda kutupa katika dampo lililopo maeneo ya Kihonda-Viwandani.
Madawa yakitolewa kwenye viroba kuteketezwa.
Kwenye uteketezaji huo, mwanahabari wetu aliwashuhudia baadhi ya maafisa wa hospitali hiyo waliokuwepo kwenye dampo hilo wakitaka tukio hilo lirushwe katika vyombo vya habari lakini wengine wakakataa na kudai libaki kuwa siri.
Ilidaiwa kuwa baadhi ya maofisa waliokuwa wanataka jambo hilo liwe siri, walikuwa wakihofia kunyimwa dawa mpya na Bohari Kuu ya Taifa (MSD).
Maaskari wakisimamia zoezi hilo.
Mwanahabari wetu alipohoji sababu za baadhi ya maofisa hao kutaka kulificha tukio hilo, walimjia juu na kumtaka afute picha za tukio hilo lakini jitihada zao zikagonga mwamba kwani paparazi wetu alifanikiwa kuwatoka.
Baadhi ya dawa zilizowekwa tayari kuteketezwa.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walihoji kulikoni kuwe na shehena kubwa ya madawa yaliyoharibika wakati wamekuwa wakitaabika wakiambiwa dawa hakuna mara kwa mara wanapokwenda hospitalini hapo?
Katapila likiandaa shimo kwa ajili ya kufukia madawa hayo.
Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Godfrey Mtei na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri kutokea na kudai dawa hizo zilikuwa zimeisha muda wake wa matumizi na hakukuwa na namna yoyote zaidi ya kuziteketeza kwa moto.
“Ni utaratibu wetu, dawa zikiharibika huwa tunaziteketeza kwa moto,” alisema Mtei