Monday, February 2, 2015

ZITTO AMTAKA WAZIRI NYALANDU KUJIUZULU AKISHINDWA KUTOA TANGAZO GAZETINI LEO JIONI

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akichangia hoja za kamati bungeni leo.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ifikapo leo jioni awe ametoa tangazo katika gazeti la serikali ili kuruhusu tozo mpya za mahoteli kwenye hifadhi la sivyo ajiuzulu cheo chake.
Sehemu ya ripoti inayoonyesha serikali inavyopoteza fedha nyingi kwa kukosa malipo ya tozo.
Zitto ameyasema hayo leo wakati akichangia kwenye majadiliano ya hoja za kamati bungeni.
Zitto amesema kuwa serikali inapoteza shilingi bilioni 2 kila mwezi kwa kitendo cha Waziri wa Utalii kutotoa tangazo katika gazeti la Serikali ili kuruhusu tozo mpya za mahoteli katika Hifadhi.
Tangu mwaka 2011 mpaka 2014, Serikali imepoteza tshs 80 bilioni.
HOTUBA YA NDG. ZITTO KABWE KWA TAARIFA YA KAMATI YA KILIMO NA KAMATI YA ARDHI
Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2014 umekuwa ni mwaka mwema kwa sekta ya kilimo nchini. Uzalishaji umeongezeka, mazao ya chakula tumezalisha ziada kwa 125% ya mahitaji yetu ya chakula. Kwa upande wa mazao ya biashara, zao la Korosho limeweka rekodi Mpya kwa kuzalisha takribani tani 200,000 za Korosho.
Hata hivyo wananchi hawana furaha na mafanikio haya kwa sababu ya kutojiandaa kwetu. Wakulima wa mahindi hawajalipwa na bado tunahangaika na soko la mahindi na mchele. Serikali bado inaruhusu Mchele kutoka nje kuingia nchini ilihali mchele wetu unakosa soko. Maghala ya kuhifadhi nafaka bado kujengwa na Serikali inasema inaongea na nchi ya Poland kupata mkopo wa kujenga maghala. Ni kama vile Serikali haikuwa na mipango wakati inajua kuwa uzalishaji utaongezeka zaidi ya maradufu.
Mheshimiwa spika,
Mwaka 2014 tunaweza kuwa tumevuka $1bn ya mauzo nje katika sekta ya kilimo kufuatia mafanikio makubwa katika Korosho na Tumbaku. 60% ya mapato ya fedha za kigeni katika kilimo yanatokana na mazao 2 tu: Tumbaku na Korosho. Mazao haya yanalimwa mikoa ya Tabora, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Katavi na Kigoma.
Ukitazama takwimu za Bajeti, mikoa hii ndio yenye kupata fedha kidogo zaidi za miradi ya maendeleo kuliko mikoa mingine nchini. Vile vile wakulima wa mikoa hii ndio wananyonywa zaidi kutokana na mfumo mbovu wa usambazaji wa pembejeo na soko la mazao yao.
Taarifa ya kamati ya PAC iliyopitishwa na Bunge wiki iliyopita inaonyesha namna mfumo wa kifisadi katika zao la Korosho unavyowaacha wakulima wa Korosho katika umasikini wa kutupwa. Wakulima wa Lindi na Mtwara wanapewa pembejeo zilizo expire na hakuna hatua inayochukuliwa.
Bado tunaendelea kuuza nje Korosho ghafi na ku export maelfu ya kazi ambazo zingefanywa na vijana na wanawake wa Mtwara. Korosho nyingi inaibiwa vijijini na vyama vya msingi havilindi maslahi ya mkulima mdogo.
Mheshimiwa spika, napendekeza kwamba sasa tuseme basi na kuacha kabisa kuuza nje Korosho ghafi. Tunapoteza wastani wa dola 115m kila mwaka kwa kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Iwapo tungekuwa tunauza Korosho iliyobanguliwa kwenda nje Tanzania ingekuwa na mapato ya fedha za kigeni zaidi ya dola 500m kwa mwaka kwa Korosho peke yake.
Napendekeza tutumie makato ya ' export levy' katika kipindi cha miaka 5 ijayo kujenga viwanda vya kubangua Korosho vijijini kwa ushirikiano kati ya vyama vya ushirika, serikali na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tumbaku naomba Serikali ilieleze bunge hatua ambazo imechukua dhidi ya viongozi wa ushirika waliotafuna fedha za wakulima wa tumbaku mkoa wa Tabora. Naibu Waziri Kilimo alitamka hapa kwamba jalada lipo kwa IGP, tuelezwe hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya ubadhirifu mkubwa huo na ni namna gani wananchi wanafidiwa kutokana na upotevu huo mkubwa wa fedha.
Mheshimiwa spika, narejea pendekezo langu kwamba Serikali ianzishe rasmi Hifadhi ya jamii kwa wakulima ili sio tu wapate mafao ya muda mrefu na wa mfupi lakini pia kuwezesha wakulima kufaidika na kilimo kwa kupata mikopo ya pembejeo na shughuli za kuongeza thamani bidhaa zao.
Akiba ya wakulima inaweza kabisa kusaidia benki ya kilimo kwa mfuko wa pensheni kwa wakulima kuwekeza hisa zake kwenye Benki hiyo na hivyo miradi mikubwa ya kilimo kuwa na chanzo cha fedha za maendeleo badala ya kutegemea Bajeti ya serikali.
Ardhi
Mheshimiwa Spika,
Kamati ya PAC imefanya uchunguzi maalumu kuhusu makusanyo madogo katika wizara ya ardhi yanayotokana na kutokuwa na rekodi sawa sawa za viwanja nchini. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alieleza katika taarifa yake ya mwaka 2012/13 kwamba, viwanja zaidi ya 263,000 jijini Dar Es salaam havipo katika rekodi ya Msajili wa hati.
Maana yake ni kwamba Serikali inapoteza mapato zaidi ya tshs 83 bilioni Kwa mwaka. Viwanja hivi vinashikiliwa na maafisa wa wizara ya ardhi. PAC imependekeza kwamba mara moja Serikali ianze kutoa Hati za Ardhi za kidigiti ( digital land titles) na kuziwianisha na nambari za utambuzi wa mlipa kodi ( TIN ).
Hatua hii itaondoa kabisa tatizo la hati zaidi ya moja kwa kiwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja. Mfumo huu uanze kwa Manispaa za Jiji la Dar Es Salaam na baadaye nchi nzima. Serikali, kwa kuwa haina Bajeti, ifanye mradi huu kwa kutumia PPP kwa kushirikisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika mapendekezo ya taarifa ya taarifa ya kamati kwa kuweka pendekezo la kuitaka Serikali kuanza mradi huu katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai mwaka huu.
Utalii
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa Waziri wa Utalii ameshindwa kutoa tangazo la Serikali ili tozo Mpya za concession zianze kutozwa. Tozo Mpya hazitozwi toka mwaka 2011 na hivyo TANAPA kupoteza zaidi ya shilingi 80 bilioni.
Wafanyabiashara walikwenda mahakamani na kushindwa kesi. Waziri miezi minne amekaa bila kutekeleza hukumu. Waziri anapaswa kuwajibishwa kwa kupotezea mapato Serikali. Bunge limuazimie Waziri huyu iwapo mpaka mwisho wa siku Leo atakuwa hajatoa tangazo la Serikali.
Zitto Kabwe