Tuesday, June 23, 2015

KIONGOZI CHADEMA ADAIWA KUUAWA KWA LIBWATA

Na Gregory Nyankaira, Butiama
LICHA ya kukataa katakata kuhusika, mwanamke aliyejulikana kwa jina la Manyaki Iseke (34), mkazi wa Kitongoji cha Mahakamani, Kijiji cha Singu wilayani Butiama, Mara ameingia katika kashfa nzito akidaiwa kumuua mumewe, Khamis Manyama (37) kwa dawa inayodaiwa ni ya kienyeji ‘limbwata’ kwa lengo la kutaka apendwe zaidi.
Mkazi wa Kitongoji cha Mahakamani, Kijiji cha Singu wilayani Butiama Khamis Manyama anayedaiwa kuuawa kwa libwata.
Mpaka kifo chake, marehemu Manyama alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Kata ya Kukilango.
Khamis Manyama anayedaiwa kuuawa kwa libwata akiwa katika picha na mkewe.
Habari kutoka kwa ndugu wa marehemu zinadai kuwa, mwanamke huyo aliyeolewa na marehemu mwaka 2009 na kuzaa naye watoto wawili, anadaiwa alinunua dawa ya mitishamba kutoka kwa mwanamke mmoja mjasiriamali anayefanya biashara zake Stendi ya Kiabakari, Butiama kisha akamuwekea mumewe kwenye chai kwa mlengo wa kuzidisha mapenzi.
......kaburi la marehemu Khamis Manyama anayedaiwa kuuawa kwa libwata.
Ikaendelea kudaiwa kuwa, baada ya mumewe kunywa chai hiyo alianza kuumwa tumbo huku likivimba sambamba na maumivu makali sehemu mbalimbali za mwili hivyo kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ambapo inadaiwa vipimo vilionesha ini  liliharibika.
 Licha ya madaktari kujaribu kumtibu, lakini mgonjwa huyo hakupata nafuu hivyo alirudishwa nyumbani ili akatibiwe kienyeji.
“Waganga walikwenda nyumbani kwake kumtibu, ndipo wakabaini kuwa, chanzo cha maradhi yake ni kuwekewa dawa ya mitishamba na mkewe kwenye chai ili kuongeza upendo.
“Marahemu aliposikia hivyo aligoma kuugulia nyumbani, akatoa wosia kwa ndugu zake kwamba akifariki dunia mwili wake usiingizwe kwenye nyumba ya mkewe na wala mkewe huyo asirithi kitu chochote,” alisema ndugu mmoja akiomba hifadhi ya jina lake.
Manyama alifariki dunia Juni 15, mwaka huu na kuzikwa siku iliyofuatia huku mazishi yake yakitawaliwa na majonzi mazito na baadhi ya waombolezaji wakitamka maneno ya kulaani waziwazi kitendo cha mwanamke huyo kumuwekea dawa mumewe kwenye chai.
Habari zaidi zinadai kuwa, ndugu wa marehemu walimtaka mwanamke huyo atakapomaliza matanga afungashe kwenda kwao.
 Uwazi lilibahatika kuzungumza na mwanamke huyo kuhusu tuhuma hizo dhidi yake ambapo alisema:
“Ni mambo tu ya waganga wa jadi walioletwa kumtibu mume wangu nyumbani ndiyo waliowaeleza ndugu wa marehemu eti mimi nilimuwekea dawa kwenye chai. Ni maneno ya kutuchonganisha tu. Lakini ukweli ni kwamba sihusiki na wala sijui lolote kuhusu kifo cha mume wangu, wananisingizia tu.
“Kama ni upendo, marehemu alikuwa akinipenda sana, sasa nilikuwa natafuta upendo gani zaidi jamani? Wale waganga wamenizushia tu.”