Tuesday, June 23, 2015

BABA ANAYEDAIWA KUMCHINJA MWANAYE HUYU HAPA

Shani Ramadhani na Mayasa Mariwata
MAPYA yameibuka! Kwamba baba mzazi anayedaiwa kumchinja mwanaye hivi karibuni maeneo ya Mabibo Luhanga jijini Dar, Maneno William Kasuga (50) (pichani),  kuwa kabla hajafanya unyama huo aliomba atumiwe pesa na mzazi mwenzie ndipo  amrudishe mtoto.
Baba aliyefahamika kwa jina la William Kasuga akionekana katika picha na mwanae aliyemchinja.
Akizungumza na waandishi wetu bibi wa marehemu William,  Mwanaidi Hassan alidai kabla ya tukio, baba mzazi aliomba arushiwe pesa na mzazi mwenzie halafu ndiyo amrudishe mtoto huku akitoa onyo kali.
“Mtoto alikuwa na baba yake tangu saa mbili asubuhi wakati huo mama yake alikuwa akimpikia uji na baada ya uji kuiva alimpigia simu mumewe ili amrudishe mtoto anywe uji halafu ndiyo aondoke naye, yule baba alisema kuwa anataka atumiwe shilingi elfu hamsini kwanza halafu ndiyo aonyeshe mtoto alipo.
“Mwanangu alijua ni utani akapiga tena kwa mara nyingine akaambiwa tena kauli ileile, akaona atushirikishe sisi na baadaye akaamua kwenda katika Kituo cha Polisi Mabibo Luhanga na kutoa taarifa lakini polisi walipouliza wakaambiwa mtoto yuko na baba yake hawakushtuka wakasema huenda anatania hivyo yeye arudi nyumbani na mtoto atarudi tu,” alisema bibi wa marehemu.
Alidai baba mzazi huyo hakuishia hapo, alipiga tena simu kwa mara nyingine huku akimuamuru mzazi mwenziye atume pesa haraka iwezekanavyo na kama atashindwa basi atakuwa amemkosa mtoto kabisa.
“Mimi nilijua hivyo kuwa atarudi tu kwa sababu huwa anamchukua na kumrudisha lakini nikashangaa alipopiga simu kwa mara nyingine tena huku akisema nimtumie hiyo pesa haraka ndani ya saa moja na kama nitachelewa basi yeye atamchinja mtoto na mimi nitakuwa nimemkosa kwa uzembe wangu.
“Nikawapigia rafiki zake na kuwaeleza kuhusu hilo wakashangaa na kuniambia huenda alikuwa amechanganyikiwa kwa sababu hata mimi ndugu zangu walianza kunijia juu na kuniambia kama alinipa hizo shilingi elfu hamsini nimrudishie nikawaambia hakunipa ndiyo nikajaribu kupiga simu ikawa haipatikani na ndipo nilipoanza kusikia minong’ono huko nje kuwa kuna mtoto amechinjwa kwenye Msitu wa Njia ya Miti uliopo pembezoni mwa Shule ya Sekondari Loyola,” alisema mama mzazi wa mtoto huyo, Amina Hassan.
Habari hii iliandikwa katika gazeti hili toleo lililopita likiwa na kichwa cha habari: ‘Baba mzazi amchinja mwanae wa kumzaa.