“Nisaidieni mwanangu awe kama watoto wengine,” ni maneno ya mama mzazi wa mtoto Azimina Abdallah (miezi 11), mkazi wa Zanzibar, Unguja anayeishi kwa mateso na maumivu makali kutokana na jicho kuvimba tangu azaliwe.
Kwa sasa mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Amina Mbaruku anahangaika naye huku baba yake akidaiwa kutoonekani kwa muda mrefu, hivyo kuchukua uamuzi wa kuiomba jamii imsaidie.
MAUMIVU MAKALI APATAYO MTOTO
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita katika Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa na Mishipa (MOI), Wodi A ya Watoto, mama huyo alisema kwamba maumivu anayoyapata mwanaye siyo ya kawaida na hata yeye hapati usingizi kutokana na mtoto wake kulia usiku kucha.
Mama huyo aliendelea kusema:
“Mwanangu nilijifungua katika zahanati iliyopo Kijiji cha Kivunje, Unguja akiwa na tatizo hili la uvimbe na kila anapokua na uvimbe pia unakua huku ukimsababishia maumivu makali. Tulihamishiwa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar baada ya hali yake kuwa mbaya.
KIPIMO CHA SH 450,000
“Mwezi wa tatu mwaka huu tulikuja Muhimbili kwa matibabu zaidi, baadhi ya vipimo vilifanyika lakini kuna kipimo kinahitajika kifanyike katika hospitali binafsi ambacho gharama yake ni shilingi laki nne na nusu fedha ambazo sina.
“Mume wangu anayefanya shughuli ya kuuza nazi alinikataza nisije Muhimbili kwa sababu hana uwezo wa kutusafirisha pia alidai hana fedha ya kunitumia kwa ajili matumizi, alinishauri nibakie kule nyumbani ili tuwe tunatumia miti shamba, sikukubali.
“Niliwaona madaktari wa Zanzibar, nilipowaeleza kwamba mume wangu hakuwa na uwezo walinisafirisha mimi na mwanangu hadi hapa Muhimbili.
“Nashukuru tumefika lakini napata shida sana hata fedha za vipimo na za kumnunulia mtoto pampasi sina.
“Nawashukuru madaktari na wauguzi wa hapa MOI wanavyonisaidia kadiri ya uwezo wao, lakini kuna huduma zingine ambazo hazipatikani hapa kama ya kipimo cha T Scan.
“Watoto wangu wengine watatu nimewaacha na mama wa kambo anayejishughulisha na kilimo cha mihogo, hata hivyo bado wana matatizo makubwa sana, baba yao tangu nimefika hapa hajawahi kunipigia simu na nimesikia ameondoka nyumbani.
Napenda kuwasiliana naye ili nimweleze kinachoendelea lakini nashindwa.
“Napata shida sana na huyu mtoto lakini nitahakikisha napambana hadi hatua ya mwisho, siwezi kumuacha kwani nampenda sana, ninachoomba kwenu Watanzania wenzangu mnisaidie ili mwanangu apone aweze kufurahia maisha kama watoto wengine wenye afya njema,” alisema mama huyo.
Kwa yeyote ambaye yupo tayari kumsaidia mtoto huyo awasiliane na mama yake au amsaidie kwa kupitia simu ya muuguzi wake Muhimbili kwa namba 0719 626520 au 0783 536320.