Shauku ya wanawake wengi kuitwa mama ni kubwa sana, namaanisha kwamba kuwa na mtoto ni moja ya heshima ambayo wanawake wengi wanaililia, walio kwenye ndoa na hata wale walio nje ya ndoa.
Lakini wakati uhalisi ukiwa hivyo, vitendo vya kutoa mimba vimekuwa vikiripotiwa kila siku. Baadhi ya wanawake wamekuwa wakijisahau na kujikuta wamenasa bila kutarajia kisha kukimbilia kutoa. Huu ni uuaji!
Na niseme tu kwamba, kama uliwahi kutoa mimba, tubu kwa Mungu wako, kama una mimba na unataka kuitoa, achana na mawazo hayo na kama hujawahi kushika mimba bila kutarajia, kuwa makini kuanzia sasa.
Kwa nini leo nAyaandika haya?
Ni kwa sababu ya ushuhuda alioutoa msanii wa filamu, Wema Sepetu kupitia Clouds TV, Kipindi cha Take One hivi karibuni. Wema alizungumza mambo mengi, alieleza jinsi alivyobeba mimba ya marehemu Steven Kanumba, akaitoa na namna uamuzi wake huo unavyomtesa.
Anahisi hatazaa tena
Kwa maelezo yake Wema anasema kuwa, tangu afanye hivyo imekuwa ni ngumu kwake kushika mimba wakati sasa anatamani sana awe na mtoto wake.
“Mimi napenda sana watoto, kila mtu anajua hilo na napenda siku moja niwe na wa kwangu. Tumehangaika sana mimi na Diamond (Nasibu Abdul) kutafuta mtoto lakini ilishindikana, ikafika wakati nikiziona siku zangu naumia. Nimehangaika hosptalini, nimetumia kila aina ya dawa lakini wapi.
Anahisi kutoa mimba kumechangia
“Wakati mwingine nahisi labda ‘abortion’ imefanywa vibaya kiasi cha kwenda kuharibu vitu huko ndani. Nilitoa mimba kwa kuwa sikuwa tayari kupata mtoto, nilikuwa mdogo na pia ndiyo kwanza nilikuwa nimeingia kwenye penzi.”
Wema anaeleza kuwa, Kanumba hakupenda kile kitendo cha kutoa mimba yake na hata kabla ya kifo chake kuna wakati alikuwa akimtania kwa kumwambia ana deni lake.
“Aliniambia kuwa ananidai na kwamba atafanya vyovyote nimrudishie watoto wake. Sasa huenda labda mzimu wake ndiyo unaosababisha haya yote,” anaeleza Wema kwa masikitiko.
Umejifunza kitu?
Ushuhuda huu wa Wema ni lazima uwe fundisho kwa kila mwenye ndoto ya kuitwa mama.
Leo unaweza kupata mimba, ukasema bado hauko tayari kuzaa, ukaitoa! Kumbe hiyo hiyo ndiyo ilikuwa chansi pekee na matokeo yake ikawa ndiyo basi tena.
Wema anafikiria hivyo lakini pia huenda ikawa tofauti na kile anachodhani kwani yawezekana ni mtihani tu ambao Mungu anampa ili ampime imani yake.
Lakini pia wapo wanawake ambao mpaka leo wanateseka kwa kutopata mimba kutokana na laana za wapenzi wao. Endapo uko kwenye uhusiano au ndoa, ukapata mimba na mwenza wako akafurahi kisha kwa sababu unazozijua wewe ukaitoa, chozi lake haliwezi kukuacha salama.
Mwanaume ataumia kwa kuifuta ndoto yake ya kuitwa baba na manung’uniko yake yanaweza kuwa laana kwako. Ndiyo maana Wema anasema, chozi la Kunumba huenda ndilo linalomtesa mpaka leo hii.
Neno kwa Wema
Hatakiwi kukosa furaha kwa kutoshika mimba. Ni kweli baada ya kutoa ile mimba ya Kanumba alihangaika sana kutafuta mtoto akiwa na Diamond lakini huenda Mungu hakupenda azae naye.
Cha kufanya ni kumtafuta mtu ‘siriasi’ wanayeweza kuanzisha familia kisha ajiachie aone kama hatanasa. Wakati mwingine hofu zinatufanya tukose amani kwa mambo ambayo huenda muda wake bado.