Majeruhi
Na Igenga Mtatiro, Tarime
Hii siyo siasa! Ndivyo walivyokuwa wakisema watu wengi mjini hapa baada ya hivi karibuni kushuhudia mtu mmoja, Mwita Bhoke Watei (37), mkazi wa Kijiji cha Nyandage, Kata ya Nyanungu, Tarime mkoani hapa, akiuawa kwa kukatwa mapanga katika vurugu za kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini kote kwa sasa.
Katika tukio hilo baya na la kulaaniwa na kila Mtanzania, baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walionesha kusikitishwa na tukio hilo wakilaani vikali vurugu za aina yoyoye na mahali popote nchini hasa wakati huu wa kampeni.
Mmoja wa mashuhuda hao, Pius Londo, mkazi wa wilayani hapa aliliambia Uwazi kuwa siasa safi ni zile ambazo hazihusishi vurugu na kwamba katika kipindi tulichonacho Watanzania wanahitaji siasa za kistaarabu.
“Hii siyo siasa hata kidogo, watu wanatakiwa kunadi sera zao na siyo kama tulivyoshuhudia, watu wanapigana kwa mapanga, mawe na visu. Huu siyo ustaarabu,” alisema Pius akikemea vikali vurugu zinazojitokeza kwenye kampeni sehemu mbalimbali nchini.
Naye Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime na Rorya, ACP Lazaro Mambosasa amekemea vikali matukio hayo huku akifafanua kuwa, pia kulikuwa na watu watano waliojeruhiwa kwenye vurugu hizo zisizo za kistaarabu.
Baadhi ya majeruhi
Aliwataja waliojeruhiwa vibaya kwa kukatwa mapanga, visu na kupigwa na mawe katika eneo la Mangucha kuwa ni pamoja na Chacha Mwita Chacha (32), mkazi wa Nyandage aliyejeruhiwa mgongoni, miguuni na mikononi wakati Kimunye Chacha Mogesi (54), mkazi wa Kegonga alijeruhiwa mikono na kichwani huku Elizabert William Marwa (43) akijeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini.
Maofisa wa polisi wakiwa eneo la tukio
Kamanda Mambosasa aliwataja wengine waliojeruhiwa sehemu mbambali wilayani hapa katika vurugu za kampeni kuwa ni Queen Ryoba (47), mfanyabiashara aliyeumizwa sehemu mbalimbali za mwili wake na Nyaitati Maranya (30), mkazi wa Kegonga alijeruhiwa mikono.
Kamanda huyo wa polisi alibainisha kuwa chanzo cha vurugu hizo katika kampeni ni wafuasi wa chama kimoja walipokuwa wakiandamana kumpokea mgombea udiwani wao ndipo wakakutana na wa chama kingine na kuanza vurugu.
Gari lilivyoharibiwa
Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Rose Hosea aliliambia gazeti hili kuwa walipokea mwili wa marehemu huyo aliyekuwa amefariki dunia baada ya kuumizwa vibaya kisha wakapokea majeruhi kadhaa.
Alimtaja aliyepewa rufaa ya kwenda katika Hospitali ya Musoma kuwa ni Chacha Matiko wakati waliopo katika hospitali hiyo ni Marwa Matiko, Buhuru Joseph na Nyaitate Maranya.
“Hakuna siasa za aina hii, nashauri vyombo vya ulinzi kuhakikisha kunakuwa na usalama wakati huu wa kampeni na sisi wananchi tujue hiki ni kipindi cha mpito hivyo tuitunze amani yetu,” alisema Rose akionesha kusikitisha na mambo ya vurugu za kwenye kampeni.
Wakati hayo yakitokea, katika Jimbo la Tarime Mjini, nako kuliibuka vurugu za watu wasiojulikana ambao walipasua vioo vya gari la mmoja wa wagombea ubunge wa jimbo hilo na kujeruhi watu wawili hivyo polisi wanawasaka wahusika ili kukomesha vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Chacha Heche, Katibu wa Chadema mkoani hapa, alilitaka jeshi la polisi kuchukua hatua kwani hivyo ni viashiria vya uvunjifu wa amani nchini na kwamba ni muhimu kuvidhibiti mapema, kauli ambayo iliungwa mkono na kiongozi mmoja wa CCM wilayani.