Tuesday, March 22, 2016

Mwanamuziki Diamond Platnumz Ateketeza Sh.Mil 100 Ulaya Akiwa na Familia yake

Kufuru! Ndilo neno pekee linaloweza kuakisi takriban Sh. milioni 100 ambazo Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameziteketeza akiwa na msururu mrefu wa wanafamilia wa Wasafi Classic Baby (WCB) barani Ulaya, akianzia nchini Ujerumani kufanya shoo sambamba na kula bata, Wikienda linakupa habari kamili.

Diamond aliyeambatana na wanafamilia kama 14 wakiwemo Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Sandra’, Tiffah (mwanaye), Romy Jons (DJ wake), Kifesi (mpigapicha), meneja (Salam), mke wa Tale (meneja Tale), madansa wanne na dada mmoja ambaye ni ndugu wa Zari, walikwea pipa na kufikia Frankfurt, Ujerumani.

TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo kilicho karibu na familia ya Diamond kilichoambatana na msafara huo kilipenyeza ‘ubuyu’ kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wake, Diamond alitenga si chini ya Sh. milioni 100 ili kufanikisha ziara hiyo aliyoipa jina la Europe Tour ambapo inatarajiwa kuchukua takriban wiki tatu.
“Diamond ni noma, ameandaa mkwanja usiopungua milioni 100 kwa ajili ya msafara wake. Fedha hizo zitatumika kuanzia usafiri wa ndege kwenda na kurudi, chakula, shopping na malazi kwa kipindi chote cha wiki tatu atakachokuwa Ulaya,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

WATUA FRANKFURT
“Walitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Frankfurt, Ijumaa (iliyopita), walichelewa kutoka uwanja wa ndege kwa sababu walikuwa na mizigo mingi lakini pia bahati mbaya kitoroli cha kumbebea Tiffah kilipotea hivyo uongozi ulichukua muda mrefu kukitafuta hadi walipokipata.”

AMEFUATA NINI NCHINI HUMO?
Chanzo hicho kiling’amua kuwa, Diamond alikuwa na ziara ya kimuziki barani Ulaya lakini kwa kuwa imeangukia wakati wa Sikukuu ya Pasaka, aliamua kuambatana na mama yake, mpenzi wake (Zari) na mwanaye ili wakainjoi.
“Ameona aitumie ziara hii ya kimuziki pia kuinjoi. Kila atakapokuwa anapita atakuwa anapata muda wa kula bata za nguvu, kufanya shopping za hapa na pale ambapo kama unavyojua tena huyu Diamond ndiyo Rais wa Wasafi, kila anapotua na msafara mzima unalala kwenye hoteli ya kifahari ambayo si chini ya nyota tatu.

SHOO ZOTE HIZI HAPA
“Jumamosi (iliyopita) ndiyo ataanza kupiga shoo Franfurt, Machi 25, atakuwa Oslo (Norway), Machi 26, atakuwa Bergen (Norway), Machi 27, atakuwa Stockholm (Sweden), Aprili 1, atakuwa Bruxelles (Belgium), Aprili 2 ni Stuttgart (Ujerumani), Aprili 8 ni Helsink (Finland) na Aprili 9 atamalizia Copenhagen (Denmark),” kilisema chanzo hicho.


SHOO ZITAFIDIA MATUMIZI?
Ijumaa Wikienda lilipokibana chanzo hicho kutaka kujua Diamond ataingiza shilingi ngapi kama malipo ya shoo hizo ili kufidia au kuzidi matumizi ya shilingi milioni 100, kilisema hakina uhakika wa malipo ya shoo kama yatafidia gharama lakini kikashauri aulizwe Diamond mwenyewe.
“Dah! Kuhusu malipo ya shoo, mimi kwa kweli sijui japo naamini lazima itamlipa, Diamond siyo mpuuzi aje huku atumie hela nyingi kuliko fedha atakazolipwa kwenye shoo. Wote atupandishe ndege daraja la kati. Atakuwa ameshafanya hesabu na kuona anabaki na faida katika ziara ndiyo maana akakubali kuja na msafara mkubwa, ila kama vipi muulize mwenyewe,” kilisema chanzo hicho.

DIAMOND HUYU HAPA
Wikienda lilimtafuta Diamond kupitia Mtandao wa WhatsApp ili kutaka alithibitishe ukweli wa yeye kuteketeza shilingi milioni 100 katika ziara hiyo ambapo alikataa kuzungumzia malipo aliyoyapata kwa shoo hizo lakini akadai kuwa zinaweza kufika au hata zaidi kulingana na starehe watakazoamua kuzifanya.

“Siwezi kusema moja kwa moja kama inafika au la lakini inaweza kufika na hata zaidi. Wewe chukulia mimi tu na familia yangu (yeye, Tiffah, Zari na ndugu zake) nimetenga kama dola 30,000 (zaidi ya Sh. milioni 65) kwa ajili ya usafiri, malazi na shopping za hapa na pale sasa vipi kuhusu timu nzima ya madansa, meneja na wengine?” alihoji Diamond.

UCHUNGUZI WA WIKIENDA
Gazeti hili lilifanya uchunguzi wa wastani wa bei ya nauli pekee kutoka Bongo hadi Ujerumani kwa daraja la chini (Economy Class) si chini ya shilingi milioni 3 kwa mtu mmoja. Daraja la kati (Business Class) si chini ya shilingi milioni 5 kwa mtu mmoja kwa maana ya kwenda na kurudi Bongo.

MCHANGANUO ZAIDI
Kama wamepanda watu wote (14) kwenye Economy Class maana yake watakuwa wametumia si chini ya Sh. milioni 42 kwa usafiri pekee. Lakini endapo watakuwa wamepanda Business Class watakuwa wametumia si chini ya Sh. milioni 70.

INAWEZEKANA!
Kama familia ya Diamond imetumia Sh. milioni 65 kwa malazi, usafiri na shopping ni zaidi ya robo tatu ya Sh. milioni 100 hivyo ni dhahiri timu iliyosalia inaweza kuwa imetumia zaidi ya Sh. milioni 30 kwa nauli, malazi na chakula, jambo ambalo halijawahi kutokea Bongo kwa staa yeyote.

Chanzo: Global Publishers