Thursday, February 12, 2015

MAUAJI YA BILIONEA MSUYA YALISUKWA HIVI...HATARI SANA


Erasto Msuya
 Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imeelezwa namna mauaji  ya ‘Bilionea wa Madini ya Tanzanite’, Erasto Msuya (43), yalivyosukwa na mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Sharif Athuman (31), ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu, mkoani Arusha.
Sharif na wenzake; Shaibu Saidi maarufu kama “Mredii” (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na Mussa Mangu (30), Shangarai kwa Mrefu ( Arusha), Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), wa Dar es Salaam na Lang’ata, wilayani
Hai, Karim Kihundwa (33), wa Kijiji cha Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu “Mjeshi”, wa Babati, mkoani Manyara, wanakabiliwa na kesi hiyo ya mauaji namba 12 ya mwaka 2014.
 
Wakili Mkuu Mfawidhi wa Jamhuri anayeongoza upande wa mashtaka, Neema Mwenda, akisaidiwa na Abdallah Chavula, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Jaji Amaisario Munisi namna ambavyo washitakiwa hao walivyokutana na kudaiwa kula njama za kutekeleza mauaji kwa kutumia mbinu shawishi za kumvutia  Msuya kukutana nao ili wamuuzie vipande vitatu vya madini ya Tanzanite.
 
“Mheshimiwa Jaji, shauri hili namba 12 la mwaka 2014; la mauaji ya kukusudia, ni kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2012; ambalo linakuja kwako kwa usikilizaji wa awali…mbele yako ni washitakiwa saba wanaokabiliwa na mauaji ya Erasto Msuya, ambao hata hivyo, nitaeleza mahakama yako namna walivyotekeleza mpango huo,” alisema Wakili Chavula.
 
Baada ya kuwasomea washtakiwa kosa la mauaji ya kukusudia linalowakabili, Wakili Chavula alieleza mpango wa mauaji hayo unavyodaiwa kusukwa tangu Julai 26, mwaka 2013.
 
Alidai mshitakiwa wa kwanza, Sharif Athuman alikutana na mshitakiwa wa pili, Shaibu maarufu “Mredii" Mererani na kumuomba amsaidie kutekeleza nia yake ya kumuua Msuya.
 
“Baada ya kukutana huko Mererani, Wilaya ya Simanjiro na kupanga mauaji hayo, Julai 27, mwaka 2013, mshitakiwa wa pili (Shaibu), wa nne
(Jalila) na wa saba (Mjeshi), walielekea Arusha mjini kukutana na mshitakiwa wa kwanza, ambaye ni mpangaji wa mauaji hayo na wakakubaliana kumtafuta mshitakiwa wa tano (Kihundwa) na mshitakiwa wa sita (Sadick) na baadaye walikubaliana kununua pikipiki mbili kwa ajili ya kazi hiyo,” alidai.
 
Vilevile alielezea namna mshitakiwa wa kwanza alivyodaiwa kufanikisha kusajiliwa kwa namba za simu zilizotumika katika mauaji hayo akizitaja kuwa ni 0682 405323, 0788 275697, 0762 436644, 0768 201041 na 0788 642417 kwa jina la Motii Mongululu Mollel.
 
 Aliendelea kudai kuwa katika mpango huo, mshtakiwa wa kwanza, alimtumia pia mtu aliyejiita, Adam Leale Mwangululu kununua pikipiki mbili aina ya Toyo, yenye namba za usajili T 316 CLV ya rangi nyekundu kwa Sh. milioni 1.7 na nyingine ya King Lion, namba T 751 CKG kwa Sh. 1, 650,000 katika duka moja, jijini Arusha.
 
“Alipokamilisha vitu hivyo, aliwaachia kazi washtakiwa...  Agosti 6, mwaka 2013, mshtakiwa wa saba, akitumia simu namba 0682 405323 alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms), Msuya kwenye simu yake namba 0763 700000, akijitambulisha kwamba yeye ni Motii Mongululu Mollel na kumweleza anayo madini ya Tanzanite na anataka kufanya naye biashara; kwa hiyo anaomba waonane. Siku hiyo hiyo, alimfuata Msuya na kumuuzia kipande kimoja cha Tanzanite," alidai   "Huyu mshitakiwa wa saba (Mjeshi) alipouza kipande kimoja, alimweleza Msuya kwamba, anavyo vipande vingine viwili vya Tanzanite na hawezi kumuuzia kwa siku hiyo, kwa sababu ni vya watu wawili na mwenzake hayupo. Baadaye akampigia tena simu akimwomba wakutane kesho yake eneo la Kia (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro). Ilikuwa Agosti 7, mwaka 2013; Msuya alifika na gari lake aina ya Range Rover lenye namba T 800 CKF na akawakuta Mjeshi na Kihundwa,” alidai Wakili Chavula.
 
Aliongeza kudai kuwa muda mfupi baada ya Msuya kuteremka  kwenye gari lake na kusalimiana na mshitakiwa wa saba, mshitakiwa wa tano, alitoa bunduki aina ya SMG yenye namba KJ 10520 aliyokuwa ameificha kwenye koti lake na kumpiga risasi na kufariki dunia.
 
Upande wa mashtaka uliendelea kudai baada ya kumuua Msuya, polisi walifika eneo la Mijohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Kia na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa chini, huku wauaji wakiwa wametelekeza maganda 22 ya risasi.
 
Alidai Msuya aliuawa majira ya saa 6:30 mchana, eneo la Mijohoroni, kando kando ya Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Kia.
Alidai polisi pia walikuta eneo la tukio, bastola yenye namba GLS 417T2 CAR 83271, mali ya Msuya na vitu vingine, ambavyo ni simu ya Samsung S5, Ifone na koti la mshitakiwa wa tano (Kihundwa) likiwa limetelekezwa mita chache kutoka eneo la tukio.
 
Pia uliionyesha mahakama hiyo vielelezo vinavyodaiwa kuwa vilitumika kutekeleza mauaji hayo, yakiwamo maganda 22 ya risasi za SMG, bastola, I phone, jaketi (koti), kofia ngumu ya pikipiki, ramani yenye mchoro wa eneo la tukio, taarifa ya uchunguzi wa daktari kuhusu kifo hicho, pikipiki mbili zilizotumika na taarifa ya uchunguzi ya mtaalamu wa silaha aliyethibitisha maganda ya risasi hizo yalitoka katika bunduki iliyowasilishwa mahakamani.
 
Aidha, upande wa mashtaka, uliieleza mahakama hiyo kwamba unakusudia kuwapeleka mahakamani mashahidi 50 wa Jamhuri na vielelezo vingine muhimu 40.
 
Upande wa utetezi katika kesi hiyo, unaongozwa na jopo la mawakili, John Lukindo anayemtetea mshitakiwa wa 4, 6 na wa 7. 
 
Wakili Majura Magafu anamtetea mshitakiwa wa pili na wa tano, huku Wakili Emmanuel Safari  mshitakiwa wa tatu na Wakili Hudson Ndusyepo mshitakiwa wa kwanza.
 
Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Amaisario Munisi, alisema  mahakama imemaliza usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo na tarehe ya kikao kijacho cha mahakama itapangwa na Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi na wadau wa pande zote watajulishwa.